Habari za Kitaifa

Mnachoka bure, CDF haiendi popote, wabunge wazomea mahakama


WABUNGE wamekosoa mahakama kufuatia uamuzi uliotangaza Hazina ya Kitaifa ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) kuwa haramu.

Wakijibu hukumu ya Ijumaa kuhusu hazina hiyo, wabunge hao waliitaja kuwa ya kisiasa zaidi kuliko ya kisheria. Waliapa kuhakikisha kuwa hazina hiyo imekita mizizi katika katiba.

Kiongozi wa wengi Kimani Ichung’wah aliwashutumu majaji hao kwa kushiriki katika shindano la umaarufu wa kisiasa kwa kutangaza NG-CDF kuwa haramu ili kuwafurahisha magavana.

“Majaji wanapotangaza kuwa kuna majukumu ya NG-CDF na yale ya magavana yanafanana, basi hiyo ndiyo lugha inayozungumzwa na Baraza la Magavana,” Bw Ichung’wah alisema.

“Sisi ni bunge inayounda sheria, ikiwa tunataka kuunda NG-CDF nyingine na kuikita  katika katiba, tutafanya hivyo. Ninataka kuwaambia majaji waache CDF ili watoto wa Kenya wapate elimu,” aliongeza.

Kiongozi wa walio wachache Junet Mohamed alisema uamuzi huo ulikuwa wa kisiasa na ulionyesha chuki ya majaji kwa Wabunge.

“Majaji wanajifanya kama wanaishi katika nchi nyingine, jinsi NG-CDF imebadilisha maisha ya watu inajulikana na kila mtu ikiwa ni pamoja na majaji, hawaendi nyumbani? hawaoni miradi ya maendeleo?” aliuliza..

Bw Mohamed alisema mahakama haitafanikiwa kuondoa CDF kwa kuwa bunge ndio  hutunga sheria na watafanya kila wawezalo ili kuhakikisha hazina hiyo haijatupiliwa mbali.

“Tutakata rufaa dhidi ya uamuzi huu, tuna mamlaka ya  kurekebisha  katiba, unaweza kutangaza NG-CDF mara nyingi upendavyo kuwa kinyume cha katiba lakini tutahakikisha kwamba CDF inasalia,” Bw Mohammed alisema.

Mbunge wa Eldas Adan Keynan aliwapuuza majaji hao akisema wabunge watasimama kidete na kukita hazina hiyo katika katiba.

Mbunge wa Rarieda Otiende Amollo aliliambia Bunge kuwa tayari wamejadili suala hilo katika kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria (JLAC) na hivi karibuni wataleta marekebisho ya katiba ili kuweka NG-CDF katika sheria.

“Mwisho wa vuta nikuvute ni marekebisho ya katiba. Tumekubali kama JLAC kwamba tutaleta marekebisho hayo,” Dkt Amollo alisema.

“Ni magavana, Seneti na baadhi ya Mashirika yasiyo ya serikali wanaotaka NG-CDF itupiliwe mbali, lazima tuwaambie kwamba hata hazina hii ikitoweka, haitaenda kwa magavana au maseneta au kwingine,” aliongeza.

Mbunge wa Dagoretti Kusini John Kiarie alisema NG-CDF imefanya miradi mingi ya maendeleo ambayo majaji hawawezi kuifutilia mbali.

“Mahakama ilikuwa na siku yao, ni siku yetu leo na tuko hapa kuwakumbusha kuwa hata majaji wanaweza kukosea. Sisi kama bunge la 13 tutaweka NG-CDF katika katiba ili iendelee kuboresha maisha ya watu,” Bw Kiarie alisema.

Mbunge wa Masinga Joshua Mbithi aliwaambia majaji wakome kuota kuwa wanaweza kwa vyovyote vile kusimamisha shughuli za NG-CDF.