SHAMBULIO: Wingu jeusi jijini
Na WYCLIFFE MUIA
KUNDI la wavamizi wanaominika kuwa magaidi lilitikisa jiji la Nairobi Jumanne baada ya kushambulia hoteli ya Dusit katika barabara ya 14 Riverside, mtaani Westlands.
Rais Kenyatta Jumatano alithibitisha kuwa watu 14 walipoteza maisha yao huku zaidi ya 700 wakiokolewa. Pia kulikuwa na majeruhi wengi waliotibiwa katika hospitali mbalimbali za jijini.
Wahalifu hao walitumia magari mawili na kuingia kimabavu katika hoteli hiyo baada ya kuwapiga risasi walinzi.
Wavamizi hao walifika katika hoteli hiyo wakiwa kwenye gari lenye nambari za usajili KCN 340E, na lingine ambalo walilipua punde baada ya kuwasili na kusababisha taharuki kubwa.
Baada ya kuwapiga risasi walinzi wa hoteli hiyo, magaidi hao walilipua magari kadhaa yaliyokuwa kwenye lango la hoteli hiyo.
Walinzi wa hoteli hiyo walioponea waliambia wanahabari kuwa, waliona wavamizi zaidi ya sita waliokuwa na bunduki kadhaa na ambao walikuwa wameziba nyuso zao.
Muda mfupi baadaye, milio ya risasi ilisikika na kuzua hofu kubwa katika hoteli ya DusitD2 na maeneo yaliyo karibu.
Moshi mkubwa uligubika eneo la kuingia katika hoteli hiyo huku waliokuwa katika ghorofa za juu wakisika wakilia “Tunavamiwa, tunavamiwa, tuokoeni!”
Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi wa Jinai George Kinoti aliwasili akiwa na kikosi kikubwa cha maafisa wa Recce, GSU pamoja na wale wa kukabiliana na ugaidi. Maafisa hao walifululiza moja kwa moja hadi kwa hoteli hiyo ambapo waliwaokoa baadhi ya watu ambao walikuwa wamekwama na wengine kujificha katika ghorofa za chini za hoteli hiyo.
Wakati huo wote, milio ya risasi ilikuwa ikisikika huku manusura zaidi waliokuwa na majeraha ya risasi wakiendelea kuokolewa na kupelekwa katika hospitali zilizo karibu.
Mwanahabari wa kampuni ya Nation Media Group, Silas Apolo ambaye alikuwa ameenda kufanya mahojiano na maafisa wa Tume ya Ugavi wa Raslimali(CRA) alisema yeye pamoja na mpiga picha mwenzake walijificha ndani ya afisi moja baada ya kusikia mlio wa risasi nje ya chumba walimokuwa.
“Bado tuko ndani ya afisi na tumeshtuka sana. Tuliwasikia wakipiga risasi kiholela huku wakijaribu kufungua mlango wa chumba ambacho tumejifungia. Simu yangu inaelekea kuzima na bado hatujaokolewa,”alisema mwanahabari huyo.
Maafisa wa polisi waliokuwa katika operesheni hiyo waliaokeza kuwepo na miili kadhaa ndani ya hoteli hiyo japo hawakutaja idadi.
KUMIMINIWA RISASI
“Tulitoa miili mitano, halafu tukarudi ndani kuokoa watu. Punde magaidi wakatuona wakaanza kutumiminia risasi. Ni kubaya sana ndani,” alisema afisa mmoja wa polisi.
Maafisa wa uokoaji walisema waathiriwa wengi wamejifungia ndani ya vyumba vya hoteli hiyo na wanakataa kufungulia maafisa wa usalama wakihofia ni magaidi.
Mwathiriwa mmoja alifariki akiendelea kupata matibabu katika hospitali ya MP Shah, eneo la Westlands.
Mwathiriwa mwingine aliyejitambulisha kwa jina Jeremy ambaye alikuwa anapeleka bidhaa katika hoteli ya DusitD2 alisema alisikia magaidi hao wakiapa kuua watu kwa Kiswahili.
“Baada ya kusikia mlipuko mkubwa na milio ya risasi niliona wanaume wanne wakisema ‘Ua hao, ua hao na nikajificha ndani ya lori nilimokua,”alielezea Jeremy.
Duru zilisema kuwa magaidi hao walikuwa wanawalenga zaidi ya raia 200 wa Amerika ambao walikuwa wanahudhuria kongamano katika hoteli hiyo.
Saa moja baada ya mashambaliano hayo kuanza, magaidi wa Al shaabab walikiri kuhusika katika mavamizi hayo.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Al Jazeera, msemaji wa Al shaabab, Abdiasis Abu Musab alikiri kuhusika kwa magaidi hao na kusema, “Tunaendesha operesheni jijini Nairobi kwa sasa. Tutatoa taarifa zaidi baadaye.”
Mamia ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi, bewa la Chiromo lililoko karibu na hoteli hiyo waliokolewa na maafisa wa usalama.
Akiongea na wanahabari mwendo wa saa kumi na mbili, Inspekta Jenerali wa Polisi Joseph Boinnet alisema wavamizi hao bado walikuwa ndani ya hoteli hiyo na maafisa wa usalama kutoka vitengo mbambali walikuwa wanapambana nao.
Duru zilisema maafisa wa ujasusi kutoka Israeli, Amerika na Uingereza walifika kusaidia wenzao wa Kenya.
Hospitali za Avenue, MP-Shah na Aga Khan zilizoko mtaani Westlands ziliwapokea waathiriwa wa mkasa huo huku zikiwarai Wakenya walio karibu kutoa usaidizi wa damu kuokoa manusura hao.
Tukienda mitamboni, mshukiwa mmoja aliyekuwa na bunduki alikamatwa huku shughuli za uokoaji zikiendelea.
Hoteli hiyo ya Dusit yenye makao yake makuu mjini Bangkok, Thailand ni maarufu sana kwa kutoa huduma za kimataifa kwa kongamano na viongozi wa kimataifa.