Habari za Kaunti

Kaunti yasota serikali kuu ikikalia Sh1.2 bilioni

Na SIAGO CECE September 27th, 2024 2 min read

SERIKALI ya Kaunti ya Kwale imelalamikia kutatizika kifedha kwa sababu ya jinsi malipo ya mrabaha wa madini yanavyochelewa.

Mrahaba huo ambao ulitarajiwa kuwa Sh1.2 bilioni kufikia mwaka wa 2023, haujatolewa tangu mwaka wa 2016 na hivyo kutatiza miradi ya maendeleo iliyonuiwa kufadhili.

Akizungumza wakati wa mkutano wa madini ulioandaliwa na Muungano wa Kwale Mining Alliance (KMA) Katibu wa Utawala katika Ofisi ya Katibu wa Kaunti ya Kwale, Bw Hassan Mwadzugwe, alisema hali hii italazimu kaunti kutafuta bajeti ya ziada ili kuziba pengo lililopo.

“Tayari tulikuwa tumeweka mipango ya kutumia fedha hizi katika miradi ya maendeleo, lakini kucheleweshwa kwa malipo ya mrabaha kumetulazimu kutafuta bajeti ya ziada ili kuziba pengo lililopo,” alisema Bw Mwadzugwe.

Diwani wa Wadi ya Gombato-Bongwe Tumaini Mwachaunga aliongeza kuwa ucheleweshaji huo umeathiri vibaya wakazi wa Kwale kwani miradi muhimu imekwama.

Mratibu wa KMA, Bw Kashi Jarmaine, alisisitiza kuwa kampuni kama Base Titanium, ambayo imekuwa ikilipa mrabaha kwa wakati, imetimiza wajibu wake, lakini serikali kuu haijatoa fedha hizo kwa wakati.

Alisema jamii, wanaharakati na wadau tofauti katika sekta ya madni wataungana ili kutafuta njia mwafaka ya kuhimiza idara husika kuhakikisha kuwa mirahaba hiyo imetolewa haraka.

Kampuni ya Base Titanium ambayo ni mojawapo ya kampuni zinazolipa kiasi kikubwa cha mrahaba nchini inatarajia kufunga mwishoni mwa mwaka huu, jamii zilizoathirika zikiwa bado hazijaokea mgao wao.

Kulingana na sheria ya Madini ya 2016, asilimia 70 ya mrabaha huo inapaswa kupelekwa kwa serikali kuu, asilimia 20 kwa kaunti, na 10 kwa jamii zinazopakana na maeneo ya uchimbaji wa madini.

Wizara ya Madini mwaka jana ilikuwa imehakikishia serikali za kaunti zinazoathirika na uchimbaji madini kuwa zitapokea mrahaba huo ili kufadhili miradi ya maendeleo.

Mkurugenzi wa Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya (KHRC), Cornelious Oduor, alisema shirika hilo litashirikiana na jamii kuhakikisha kuwa mrahaba huo umefikia jamii.

“Ni muhimu kuwa jamii wapate manufaa kutoka kwa madini ambayo inatolwa kwenye ardhi yake. Tayari kumekuwa na na hasara kubwa kuna watu ambao wamepoteza maisha kwa sababu ya huduma duni za afya, ilhali fedha za mrabaha zingeweza kutatua matatizo haya,” Bw Oduor.

Mapema wiki hii, Gavana wa Kwale, Bi Fatuma Achani, aliwaomba wakazi wawe na subira kuhusu utekelezaji wa miradi akisema kuna changamoto za kifedha.

Kwenye taarifa aliyotoa baada ya kufungua shule ya chekechea ya Jeza B eneo la Tsimba/Golini, Bi Achani alisema matatizo hayo yanasababishwa na jinsi fedha zinachelewa kutumwa kutoka kwa serikali ya kitaifa.

Licha ya hayo, alisema kaunti imejitahidi na kupiga hatua kubwa katika kuendeleza sekta ya elimu huku akiwataka wakazi kupuuza watu wanaokosoa kaunti bila sababu za msingi.