Kipyegon alivyofunga msimu kwa kushamiri Amerika
BINGWA wa dunia, Olimpiki na Diamond League mbio za mita 1,500, Faith Kipyegon alifunga msimu kwa kuzoa taji la riadha za wanawake pekee za Athlos NYC ugani Icahn, New York usiku wa kuamkia Ijumaa, Septemba 27, 2024.
Kipyegon alifyatuka katika mita 400 za mwisho na kutwaa taji la mbio hizo za kuzunguka uwanja mara tano kwa dakika nne na sekunde 4.79 pamoja na tuzo ya mshindi ya Sh7.7 milioni.
Alifuatiwa kwa karibu na Muethiopia Diribe Welteji (4:05.58), Mkenya Susan Ejore-Sanders (4:06.25), Muethiopia Gudaf Tsegay (4:06.81), Mwamerika Cory McGee (4:07.09) na Muingereza Katie Snowden (4:07.57), mtawalia.
Bingwa wa dunia mbio za mita 800, Mary Moraa naye aliridhika na nafasi ya pili katika kitengo chake alipofika utepeni kwa dakika 1:58.05. Alimaliza katikati ya Muethiopia Tsige Duguma (1:57.43) na raia wa Jamaica, Natoya Goule-Toppin (1:58.63).
Wakimbiaji waliokamata nafasi sita za kwanza walitia mfukoni tuzo ya Sh7,740,000 (Dola za Amerika 60,000), Sh3,225,000 (Dola za Amerika 25,000), Sh1,290,000 (Dola za Amerika 10,000), Sh1,032,000 (Dola za Amerika 8,000), Sh645,000 (Dola za Amerika 5,000) na Sh322,500 (Dola za Amerika 2,500), mtawalia.
Vitengo vilivyowaniwa ni mbio za mita 100, 200m, 400m, 800m na 1,500m. Marie-Josee Ta Lou-Smith (Cote d’Ivoire) alishinda mbio za mita 100, Mwamerika Brittany Brown akaibuka mshindi wa mbio za 200m, naye Marileidy Paulino kutoka Jamhuri ya Dominican akatawala mbio za 400m. Jasmine Camacho-Quinn kutoka Puerto Rico alikamata nafasi ya kwanza katika 100m kuruka viunzi.
Kipyegon pamoja na bingwa wa Olimpiki mbio za 5,000m na 10,000m, Beatrice Chebet walikuwa miongoni wa watu 20 waliopokea tuzo za kifahari kwenye hafla ya Golden Plate mjini New York, Amerika usiku wa kuamkia Jumanne, Septemba 24, 2024.
Kipyegon na Chebet walipokea tuzo ya kifahari ya Academy of Achievement mbele ya mshindi wa tuzo hiyo wa kitengo cha Huduma kwa Jamii mwaka 2022, Rais William Ruto.
“Nafurahia na ni heshima kubwa kupokea tuzo hii…Tuzo hii ni motisha kubwa kwa bidii, kujitolea na mafanikio tumepata,” akaandika Kipyegon kwenye mitandao yake ya kijamii.
Mshikilizi huyo wa mataji mengi ya Olimpiki ya 1,500m (matatu) na rekodi za dunia za 1,500m (dakika 3:49.04) na maili moja (4:07.64) alikuwa katika orodha ya watimkaji 36 walioalikwa kushiriki Athlos NYC.
Mashindano hayo ya mwaliko ya wanawake pekee yanadhaminiwa na Alexis Ohanian, mume wa mwanatenisi Serena Williams.