Habari za Kitaifa

Mamia ya Wakenya roho mikononi vita vikichacha Lebanon

Na MERCY SIMIYU September 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MAMIA ya Wakenya wamekwama Lebanon kutokana na mashambulio ya mara kwa mara yanayotekelezwa na Israeli dhidi ya kundi la wanamgambo wa Hezbollah.

Hata hivyo, mnamo Alhamisi, Septemba 26, 2024, serikali ilisisitiza kuwa Wakenya wote wako salama nchini Lebanon bila kufafanua ikiwa kulikuwa na mipango ya kuwahamisha hadi sehemu salama.

Halima Mohamud, Balozi wa Kenya, ambaye anahudumu kutoka Kuwait, aliambia Taifa Leo kwamba ubalozi wake unawasiliana na Wakenya wote waliokwama nchini Lebanon na kwamba walikuwa wamepewa nambari ya simu ya kumpigia endapo hatari itatokea.

“Hakuna Mkenya aliyefariki au kujeruhiwa. Tunawasiliana nao,” alisema.

‘Tuna nambari ya simu na tuko tayari kusaidia wakati wowote.’

Lakini wale waliokwama Lebanon wanatoa taarifa tofauti.

Wanadai kuwa walikuwa wametoa habari inayohitajika lakini hawajapokea mawasiliano yoyote kutoka kwa mamlaka tangu wakati huo.

Wale waliokwama ni wafanyakazi, wengi wao wakiwa wanawake, ambao walienda Lebanon kufanya kazi za nyumbani.

Kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje na Masuala ya Diaspora, angalau Wakenya 26,599 wako Lebanon.

Mnamo Oktoba mwaka jana, Wakenya 1,500 walipewa kazi nchini Lebanon kama sehemu ya makubaliano kati ya mashirika mbalimbali na Chama cha Kitaifa cha Biashara na Viwanda (KNCCI).

‘Nilikuja hapa mwaka jana, nikiwa na matumaini nikiamini maisha yangu yatabadilika lakini sasa, mambo yamekuwa kinyume na matarajio yangu,”

‘Ni kana kwamba serikali yetu imetusahau, ikituacha tukihisi kama hata hatufai – kana kwamba hatuonekani, tumesahaulika. Tunajaribu lakini mambo yanaendelea kuwa mbaya kila siku. Mabomu yanaanguka kila mahali. Jana tu, moja ililipuka karibu na nyumba yangu hivi kwamba jengo lote lilitikisika. Naishi kwa hofu nikisubiri kifo changu,” alisema Sharon Akinyi, 31, mlezi.

Mashambulio ya mabomu yalianza wiki iliyopita wakati Israeli ilipoanzisha mashambulio dhidi ya Hezbollah, ambayo inawatuhumu kwa kuwatishia wakazi karibu na mpaka na Lebanon.

Hezbollah inashirikiana na kundi la wanamgambo wa Hamas Gaza, ambalo Israeli imepigana nalo kwa mwaka mmoja uliopita wakati kundi hilo la wanamgambo lilipofanya mashambulio ambayo hayajawahi kushuhudiwa dhidi ya Israeli mwezi Oktoba 2023.

Takriban watu 400 wameuawa nchini Lebanon tangu mashambulio hayo kuanza.

Baadhi ya Wakenya walidai waajiri wao walifungia hati zao za kusafiria walipokuwa wakitoroka maeneo ya mashambulio ya mabomu, na kuwaacha.

Mnamo Julai, serikali ya Kenya iliwataka Wakenya kujaza fomu yenye maelezo ya kina ikiwa ni pamoja na anwani zao na mawasiliano ya simu.

‘Miezi imepita, na inaonekana kama tumesahauliwa. Hatujapokea habari zozote,”

‘Ni kama tumesahaulika kabisaa. Wanawezaje kutuleta huku kisha kutuacha hapa tukiwa tumekwama na kuishi kwa hofu? Hakuna mtu anayesema chochote, na inanifanya nihisi nimesahaulika sana. Wasichana wengine bado wanafika hapa, hawajui kabisa watakachokutana nacho,” alisema Alice Kalekye, ambaye anafanya kazi kama mlezi Beirut.