Kinara wa Iran Ayatollah Khamenei alaani Israel kwa kuua mkuu wa Hezbollah Hassan Nasrallah
BEIRUT, LEBANON
MAJESHI ya Israel (IDF) Jumamosi yalitangaza kuwa kiongozi wa wanamgambo wa Hezbollah Hassan Nasrallah aliuawa kwenye shambulizi lililotekelezwa mnamo Ijumaa usiku.
Nasrallah hajaonekana hadharani kwa miaka mingi kutokana na hofu kuwa angeuawa na majeshi ya Israel.
Amekuwa akifadhiliwa kuendeleza vita dhidi ya Israel na Iran.
Kiongozi huyo wa wanamgambo hao anafahamika sana Mashariki ya Kati kutokana na mikakati ya kivita ambayo amekuwa akiendeleza ili kuangamiza Israel na maadui wa Lebanon akiwemo Amerika.
IDF ilitangaza kuwa Nasrallah aliuawa wakati mabomu yalirushwa katika makao makuu ya Hezbollah ya Dahieh kusini mwa Beirut.
Jeshi hilo pia lilisema kamanda wa Hezbollah ukanda huo wa Kusini pia aliuawa wakati wa shambulizi hilo.
Nasrallah amekuwa akiongoza Hezbollah tangu 1992 na amekuwa akiwateua makamanda waaminifu kwake ambao wamesaidia kundi hilo la wapiganiaji kujijenga kutika kundi dogo hadi kubwa la kutishia na kukabili Israel.
Amerika, ambayo pia imekuwa ikiiunga Israel na kurejelea Hezbollah kama kundi la kigaidi Lebanon, nayo ilisema bado haijui iwapo Nasrallah aliuawa jinsi ambavyo Israel ilikuwa ikidai.
Kutokana na madai ya Israel kuwa walimuua Nasrallah, wengi wanasubiri kuona mwelekeo ambao Iran itachukua na iwapo sasa itaendeleza vita dhidi ya Israel moja kwa moja.
Hapo jana kiongozi wa dini Iran Ayatollah Khamenei alitoa taarifa lakini hakumtaja Nasrallah, taarifa ambayo ilifasiriwa kuwa sasa inathibitisha kiongozi huyo wa kivita huenda aliuawa kwa kweli.
Khamenei alikashifu Israel kwa kuwaua raia wa Lebanon akisema ni tabia ya uoga na kijinga.
Alitetea Hezbollah na kuyaambia majeshi ya Israel kuwa yapo mbali sana katika kuharibu au kutokomeza kundi la Hezbollah.
Pia aliwaomba Waislamu wote waendelee kusimama imara nyuma ya Lebanon na Hezbollah katika kukabili uimla na udikteta wa Israel dhidi yao.