Dimba

Mshangao mechi kubwa baina ya Shabana na Posta Rangers ikikosa kufanyika

Na WYCLIFFE NYABERI September 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MECHI ya ligi kuu baina ya Shabana FC na Posta Rangers, iliyokuwa imeratibiwa kuchezwa Jumamosi katika uga wa Gusii haikuchezwa ilivyopangwa baada ya waamuzi kukosa kufika uwanjani.

Sababu za wasimamizi hao kutofika hazikujulikana mara moja.

Lakini ilidaiwa pakubwa kuwa baadhi ya maafisa katika shirikisho la soka nchini (FKF) hawakufurahishwa na hatua ya timu ya Shabana kukata rufaa ili kuweka kando adhabu dhidi yake kufuatia uhuni wa mashabiki wake.

FKF ilikuwa imewapata mashabiki wa Shabana na hatia kwa uharibifu wa mali uliotokea Jumapili iliyopita katika uwanja wa Ulinzi Sports Complex.

Kufuatia uharibifu huo, FKF iliitaka Shabana kucheza mechi zake tano za nyumbani bila mashabiki. Pia iliwaamuru kugharamia uharibifu huo, lakini timu hiyo ilikata rufaa iliyoweka kando vikwazo hivyo kwa muda.

Kwa kuwa timu hiyo yenye makazi yake mjini Kisii ilikuwa inarejea katika uga wake wa Gusii kwa mara ya kwanza ikishiriki ligi kuu baada ya miaka 18, ilitoa rai mashabiki wake wahudhurie mechi hiyo kwa wingi na wakaujaza sawa sawa.

Lakini mashabiki hao waliojaza uwanja huo ambao ulitamatika kukarabatiwa hivi karibuni, waliachwa vinywa wazi ilipobainika kuwa mechi hiyo haitachezwa.

Mashabiki waanza kuondoka uga wa Gusii, baada ya kubainika kwamba mechi bab’kubwa baina ya Shabana na Posta Rangers haitachezwa. Shabana ilikuwa icheze mechi yao ya kwanza nyumbani baada ya kuwa kwenye kibaridi cha Ligi Kuu kwa miaka 18. Picha|Wycliffe Nyaberi

Akizungumza baada ya mchezo wao kutibuka, kocha wa Shabana Sammy “Pamzo” Omollo alisema kitendo cha FKF kutotuma waamuzi kilikuwa cha kushangaza na cha aibu.

“Kwa hakika hatujui ni nini kinaendelea. Tulipoanza kupiga jaramba, habari mseto zilikuwa zinatufikia kuwa marefa wamo njiani, ya kwamba wamechelewa kidogo. Wengine walituambiwa kuwa wamo katika vyumba vya kubadilisha na wengine walituambiwa kuwa wamezuiwa kuingia uwanjani. Hizi ndizo habari tulizokuwa tunazipata hadi kufikia mahali tuliambiwa hakuna mchezo,” kocha Omollo alisema.

Semi kama hizo zilitolewa na mwenzake wa Posta Rangers Bernard Kawinzi.

“Mimi pia sijui kwa nini mechi hii haijachezwa na ni kwa nini marefa hawakufika. Tulisafiri kuja Kisii na mandhari ni mazuri, uwanja pia umekubali lakini tunapoambiwa hatuchezi, huwa tunashangazwa na kile kinachoendelea katika soka yetu,” Kawinzi alisema.

Peter Makori, Shabiki sugu wa Shabana alisema moyo wake uliatuka baada ya kulipia tikiti ya kutizama mechi lakini hakupata nafasi ya kuona timu hizo zikimenyana.

“Ni nani atakayeturudishia pesa zetu. Tumeharibu muda wetu bure kuja hapa. Hili ni jambo la aibu,” Makori alisema.