Habari za Kitaifa

Wizara ya ardhi yakana kuwa hatimiliki 367 ziliibwa, yasema ni karatasi tu ziliporwa

Na CHARLES WASONGA September 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WIZARA ya Ardhi imekana ripoti kwamba hatimiliki 367 zimeibiwa ikifafanua kwamba karatasi maalum zinazotumiwa kuchapisha hati hizo za umiliki wa ardhi ndizo ziliibiwa katika afisi za Mchapishaji wa Stakabadhi za Serikali.

Kwenye taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Septemba 28, wizara hiyo ilifafanua kuwa karatasi hizo, zenye alama za kiusalama, huwasilishwa kwao na asasi hiyo.

“Tungependa kueleza kuwa karatasi zilizoibiwa zinaweza tu kuwa hatimiliki baada ya kuwasilishwa kwa Wizara ya Ardhi, kujazwa maelezo ya wamiliki wa ardhi, kupigwa muhuri rasmi na kuwekwa sahihi ya Msajili wa Ardhi baada ya taratibu hitajika kufuatwa,” Wizara ya Ardhi ikaeleza.

“Msukumo wa wazi wa wizi wa karatasi hizo ulikuwa nia ya magenge ya walaghai kutengeneza hatimiki feki”, ikaongeza.

Wizara hiyo ilitoa ufafanuzi huo baada ya serikali kutangaza kupotea kwa hadi hatimiliki 367 za ardhi.

“Notisi inatolewa kwa umma kwamba hatimiliki zenye nambari za utambulisho kati ya 5253001 hadi 5253367 zimeibiwa. Serikali haitahalalisha shughuli zozote zitakazoendeshwa kutumia hatimiliki hizo na kwa mujibu wa notisi hii stakabadhi hizo zimefutuliwa mbali,” akasema Abdi Hassan Ali, kwenye ilani katika gazeti rasmi la serikali toleo la Septemba 27.

Bw Ali ni afisa katika afisi ya Mchapishaji wa Stabadhi za Mchapishaji wa Serikali.

Wizara ya Ardhi ilisema kuwa imepata habari kuwa afisa mmoja katika afisi ya mchapishaji wa serikali amekamatwa na maafisa wa usalama kuhusiana na wizi huo.

“Kwa hivyo, tunatoa hakikisho kwamba taratibu zetu za utoaji hatimiliki ni salama. Wizara ya Ardhi imeimarisha juhudi zake za kupambana na ufisadi kuhusiana na shughuli za umiliki wa ardhi nchini. Inafanya hivyo kwa ushirikiano na vikosi vya usalama huku ikihakikisha kuwa karatasi zilizoibiwa hazitumiwi kuendeleza uovu katika umiliki wa ardhi,” ikaongeza.

Ripoti kuhusu wizi wa karatasi hizo za kuchapisha hatimiliki inajiri mwezi mmoja baada ya wapelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kukamata washukiwa sita kuhusiana na tuhuma za kuwalaghai Wakenya kutumia stakabadhi feki za ardhi.

Kulingana na ripoti ya polisi, washukiwa waliokamatwa katika eneo la Ngara, Nairobi ni sehemu ya genge la walaghai ambao huwapokonya Wakenya ardhi zao kwa kubadilisha maelezo ya umiliki katika faili za kawaida na jukwaa la kidijitali.

Wapelelezi walisema sita hao walipatikana wakichapisha stakabadhi ghushi za umiliki wa ardhi  katika afisi zao zilizoko mtaa huo wa Ngara.

Wakati wa operesheni hiyo maafisa hao walifaulu kunasa vitu kadhaa katika nyumba za washukiwa hao miongoni mwa vitu hivyo vikiwa hatimiliki 1, 000 ambazo hazijapigwa chapa.