Habari za Kitaifa

Sh337 milioni za Olimpiki ya Paris 2024 zilitengwa ili kuporwa?

Na DAVID MWERE September 30th, 2024 2 min read

WABUNGE wamemulika serikali kuhusiana na utata unaozingira matumizi ya Sh337 milioni chini ya Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Urithi, wakisema huenda zilitengwa ili kupora mali ya umma.

Katibu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Urithi, Ummi Bashir, alikabiliwa na wakati mgumu kushawishi Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Spoti na Utamaduni, jinsi ilivyolazimu kutumia Sh200 milioni katika maonyesho ya Kenya House, jijini Paris, Ufaransa, ili kupigia debe Kenya katika Mashindano ya Olimpiki 2024, yaliyokamilika majuzi Paris.

Wanakamati walikereka walipogundua kitita cha Sh70 milioni kilitengewa kuunda vazi la Kenya, Sh55 milioni zikatumika katika sherehe za Sikukuu ya Kiswahili zilizofanyika majuzi huku Sh12 milioni zikitumika katika ufunguzi wa sherehe za haki za walio wachache.

Matumizi hayo yanayotiliwa shaka yalitokana na Hazina ya Kupigia Debe Utalii (TPF).

Ingawa mwenyekiti wa Kamati Dan Wanyama (Mbunge wa Webuye Magharibi) hakuwa na tatizo na jumba la maonyesho Ufaransa, kamati yake ilitofautiana ikisema hatua hiyo,”haikutumia raslimali za umma kwa njia bora.”

“Wazo la kuweka Jumba la Kenya jijini Paris wakati wa mashindano ya Olimpiki lilikuwa bora. Nilibahatika kuzuru kituo hicho na ninaweza kuthibitisha kulikuwa na halaiki ya watu waliozuru wakitaka kujua zaidi kuhusu taifa letu,” alisema Bw Wanyama.

“Kwa sababu hiyo, Kenya inatarajiwa kuvuna pakubwa kupitia utalii kwa kuwa idadi ya watalii watakaotembea itaongezeka,” alisema ingawa Mbunge wa Yatta, Robert Basil, hakushawishika.

“Sielewi ni vipi Kenya ilinufaika kutokana na mpango wa mauzo wenye thamani ya Sh200 milioni. Yeyote aliyeidhinisha matumizi ya kiasi hicho cha fedha anastahili kuchunguzwa na kushtakiwa,” alisema Bw Basil.

“Olimpiki imekuwa ikitumika kuiba fedha za umma na suala hili halifai kusahaulika.”

“Safari hii maafisa waroho serikalini walishindwa kupora hela kupitia ufadhili wa wajumbe wasiohitajika lakini wakaamua kutumia Kenya House kama njia ya kufyonza fedha za umma,” alisema Mbunge wa Webuye Magharibi.

Matumizi ya fedha kwenye maonyesho ya Kenya House yalitekelezwa na Makavazi ya Kitaifa Nchini (NMK) chini ya agizo la Wizara.

“Namna ambavyo hazina hiyo inaendeshwa na kiwango cha uzingatiaji sheria zinazohitajika kufikia hazina hiyo zinafanya iwe vigumu kuwepo mianya yoyote katika matumizi na ripoti ya fedha,” alihoji Bi Nashir.

Hata hivyo, wanakamati walionyesha kutoridhishwa kwao kuhusu matumizi “yenye utata” wakiungana kuhoji Sh70 milioni zilizopangiwa kutumika kwa vazi la kitaifa na Sh55 milioni zilizotumika zote kuandaa sherehe za Sikukuu ya Kiswahili.