Makala

INAYAT KASSAM: Mzalendo halisi wakati wa mashambulizi ya kigaidi

January 16th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

BW Inayat Kassam amewavutia Wakenya wengi kwa ujasiri wake namna alijitokeza Jumanne kuwaokoa Wakenya ambao walivamiwa katika hoteli ya Dusit, eneo la Riverside, licha ya kuhatarisha maisha yake mwenyewe.

Bw Kassam, ambaye pia aliwaokoa watu wakati wa vamizi la 2013 eneo la Westgate, wakati huu alirejea kwa uzalendo na ushujaa wake, akionekana na bunduki, bila magwanda ya kujikinga risasi akishiriki uokozi Jumanne.

Bwana huyo ambaye ni mtaalam wa masuala ya bunduki mbeleni ameeleza kuwa nafsi yake humsukuma kujituma katika mazingira magumu ya aina hiyo, jambo ambalo alidhihirisha Jumanne.

Mwaka uliopita, wakati wa Kenya kuadhimisha miaka mitano tangu vamizi la Westgate lilipotekelezwa, Bw Kassam alieleza runinga ya Citizen kuwa japo anahofia usalama wake anapoenda katika mazingira ya aina hiyo kuwaokoa watu “msukumo wa kuwaokoa watu zaidi hauniruhusu kukaa tu.”

Jumanne, alikuwa mmoja watu waliowasili eneo hilo mara ya kwanza na kusaidiana na walinda usalama kuokoa mamia ya watu.

Bw Kassam ana leseni ya kumiliki bunduki, ni mkufunzi wa utumiaji bunduki na amekuwa akitoa mafunzo kwa watu kuhusu namna ya kufanya kazi na silaha hizo.

Vilevile, ndiye mtumizi na mkufunzi wa silaha peke yake aliye na leseni barani Afrika na nje ya Afrika Kusini.

Wakati milio ya risasi na milipuko ilikuwa ikitawala angani eneo la Riverside Jumanne, Bw Kassam alikuwa akionekana akiingia jengoni kifua mbele, kisha muda mfupi baadaye akitoka nje na watu aliookoa.

Mavazi yake yalikuwa na damu aidha, kutokana na kubeba ama kushika baadhi ya watu ambao walijeruhiwa.

Tangu kisa hicho, bwana huyo amejizolea sifa kemkem kutoka kwa Wakenya, wakifurahishwa na ujasiri na uzalendo wake.