HabariHabari za Kitaifa

Hakuna kupumua kwa Gachagua korti ikikosa kuzima hoja ya kumtimua

Na SAM KIPLAGAT September 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA Kuu imekataa kuzima Bunge la Kitaifa kuanza mchakato wa kumng’oa madarakani Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa UDA, Cleophas Malala, Jumatatu alienda korti kuzima kuanzishwa kwa mchakato wa kumuondoa ofisini Bw Gachagua akisema Bunge halikuzingatia usawa wa jinsia ilhali linaendelea kuendesha shughuli zake.

Jaji wa Mahakama Kuu Bahati Mwamuye alitaja kesi hiyo kama ya dharura na kuagiza wahusika wafike mbele yake Oktoba 10 kupata mwelekeo zaidi.

“Natambua kuwa kesi imewasilishwa kortini kusaka amri ya dharura na pia ya kudumu ili kuzima Bunge la Kitaifa kupokea, kujadili au kusimamia hoja ya kumbandua madarakani Naibu Rais wa Kenya,” ilisema amri ya korti.

Hata hivyo, Jaji Mwamuye hakutoa amri ya kuzuia hoja hiyo kuwasilishwa.

Uhusiano baina ya Rais William Ruto (kulia) na Naibu Rais Rigathi Gachagua umeingia mdudu na hawapatani tena, huku juhudi za kumuondoa  naibu huyo zikichacha. PICHA | PCS

Hoja ya kumtimua Bw Gachagua huenda ikawasilishwa bungeni wiki hii baada ya wabunge wanaotaka kumbandua kusema wamepata saini zinazotosha kuanza mchakato huo.

Wabunge wanamshutumu kwa kueneza siasa za ukabila, kutatiza uongozi wa Rais Willliam Ruto na pia kwa madai ya kufadhili maandamano dhidi ya serikali kati ya Juni na Julai 2024 ambapo Bunge lilivamiwa.

Wiki jana, wanasiasa watano pamoja na msaidizi wa Bw Gachagua walielekea kortini na kupata amri ya kuzuia kukamatwa na kufikishwa kortini. Hii ni baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Igonga kuidhinisha mashtaka dhidi yao.

Kwenye kesi aliyowasilisha Jumatatu, Bw Malala alisema Bunge lipo mamlakani kinyume cha sheria kwani halijazingatia usawa wa jinsia. Alieleza kwamba asasi hiyo imefeli kuhakikisha kuwa theluthi moja ya wabunge ni wanawake jinsi inavyoagiza katiba ya Kenya.

Kumwondoa Naibu Rais mamlakani, lazima hoja hiyo iungwe mkono na theluthi mbili ya wabunge na pia maseneta.