HabariHabari za Kitaifa

Hata sisi tumekuchoka! Wabunge wa Mlima Kenya waambia Gachagua

Na GEORGE MUNENE September 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WABUNGE wanne kutoka Mlima Kenya wameunga mkono kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, lakini wakaomba nafasi yake bado ipewe kiongozi kutoka eneo hilo.

Wakiongea Jumapili katika Kanisa la KAG Sagana, Kaunti ya Kirinyaga, wabunge hao walisema Bw Gachagua amedhihirisha kwamba hana heshima kwa bosi wake Rais William Ruto.

Wanne hao George Kariuki (Ndia), Elijah Njoroge (Gatundu Kaskazini), Kwenya Thuku (Kinangop) na Irene Njoki (Bahati) walisema hawana tatizo lolote hata Bw Gachagua akifurushwa serikalini.

“Hatuna shida na jitihada za kumbandua Bw Gachagua, ilmradi nafasi hiyo ipewe kiongozi kutoka Mlima Kenya,” akasema Bw Njoroge.

Mbunge wa Gatundu Kusini, Elijah Njoroge Kururia, awali mwaka jana. PICHA | DENNIS ONSONGO

Wanasiasa hao walimtaka Naibu Rais akome kuhadaa umma kwamba Rais Ruto alipata uungwaji mkono eneo la Mlima Kenya kutokana na juhudi zake (Bw Gachagua) wakati wa kampeni.

“Rais Ruto angechaguliwa Mlima Kenya hata iwapo Bw Gachagua angekataa kumuunga mkono,” alieleza Bw njoroge huku pamoja na wenzake wakiapa kuendelea kuunga serikali iliyopo, Naibu Rais apende asipende.

“Tutasalia serikalini na kumuunga mkono Rais. Kama babako amemoa mwanamke mwingine huwezi kumtoroka,” akaongeza Bi Njoki.

Wabunge hao walimshauri Bw Gachagua aridhiane na bosi wake badala ya kumshutumu hadharani kupitia mikutano ya kisiasa Mlima Kenya.

“Naibu Rais ana nambari ya simu ya Rais. Itakuwa vyema akimpigia simu ili watatue tofauti zao badala ya kuzianika hadharani,” alihoji Mbunge wa Kinangopo, Bw Thuku.

Mwenzake wa Ndia, Bw Kariuki, aliongeza kwamba Rais Ruto ndiye kiongozi wa nchi na anastahili kuheshimiwa.