Dimba

Bodi ya Man-U yazidi kuamini Ten Hag licha ya mashabiki kufoka

Na JOHN ASHIHUNDU, MASHIRIKA September 30th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MANCHESTER United imeonyesha dalili za kuendelea kuamini kocha Erik ten Hag katika mechi mbili zijazo dhidi ya FC Porto katika Europa League na Aston Villa ligini, licha ya shinikizo za mashabiki wanaotaka apigwe kalamu baada ya kikosi hicho kuchapwa 3-0 na Tottenham Hotspur kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Jumapili.

Kocha huyo raia wa Uholanzi ameshindwa kufikia kiwango cha Mikel Arteta na Pep Guardiola wanaoendelea kushindana kwenye mbio za kuwania ubingwa wa ligi hiyo, baada ya Jurgen Klopp kuondoka mwishoni mwa msimu uliopita.

Hata Arne Slot aliyechukuwa nafasi ya Klopp katika klabu ya Liverpool na Enzo Maresca anayenoa Chelsea wameonekana kuwa wapinzani wakubwa kwenye vita vya kuwania ubingwa huo, lakini ten Hag ambaye amekuwa na muda mrefu wa misimu mitatu Old Trafford tangu 2022 akizidi kusuasua.

Dhidi ya timu kubwa ligini, Manchester United tayari imekutana na Liverpool na kukubalia kichapo cha 3-0 na baadaye kulimwa 3-0 na Spurs. Swali ni je, Ten Hag ataweza Arteta na Guardiola ambao ni wazoefu kwenye ligi hiyo pamoja na Enzo wa Chelsea ambaye kikosi chake kinaimarika kila wakati?

Kikosi chake kilipochapwa 1-0 na Arsenal, Ten Hag alitoa kijisababu kwamba wachezaji wake muhimu walikuwa na majeraha, ndipo akawachezesha makinda kadhaa wasiokuwa na ubora mkubwa. Kwenye mechi 21 dhidi ya timu sita kubwa kwenye EPL, Ten Hag ameshinda mara sita tu na kutoka sare mara tano na kujivunia pointi 23 pekee.

Aliposaini mkataba mpya mwezi uliopita, Afisa Mkuu wa United, Omar Berrada alisema kocha huyo anaungwa mkono na bodo nzima ya klabu hiyo, lakini inavyoenda, huenda hali yake ya baadaye ikaamuliwa kufuatia matokeo ya mechi zijazo dhidi ya Porto na Aston Villa kabla ya likizo ya wiki mbili kupisha mechi za kimataifa.

Kufikia sasa, hakuna mchezaji wa United aliyefunga zaidi ya bao moja ligini, huku Marcus Rashford, Amad Diallo, Joshua Zirkzee, Matthijs de Ligt na Alejadro Garnacho wakiwa moja kila mmoja.