Morara Kebaso kusota seli ghadhabu zikitanda kufuatia kukamatwa kwake
WAKILI Gen Z na mwanaharakati Morara Kebaso ambaye anafahamika sana kwa kufichua jinsi mabilioni ya pesa hutumika kwenye miradi hewa na iliyokwama, Jumatatu jioni alitiwa nguvuni na polisi.
Kukamatwa kwa Bw Kebaso kulichemsha mitandao huku maelfu ya Wakenya wanaomfuatilia wakionyesha ghadhabu zao.
Kebaso, 28, alinyakwa kutoka kwa afisi zake mtaani Kahawa Sukari kisha akatupwa kwenye gari aina ya Subaru Forester.
Alipelekwa katika makao makuu ya polisi eneo la Nairobi. Video iliyonaswa na wapiga picha wa wakili huyo zilionyesha kuwa nambari ya usajili ilikuwa KCQ 166J.
Seneta wa Kisii Richard Onyonka ni kati ya walioghadhabishwa na jinsi ambavyo Bw Kebaso alinyakwa na akashutumu serikali kwa kuruhusu watu kukamatwa kiholela nchini.
“Inashangaza kuwa watu wananyakwa na kupotea kiholela nchini. Morara lazima awaachiliwe au awasilishwe kortini saa chache zijazo la sivyo serikali hii itapoteza uhalali wake kabisa,” akaandika Bw Onyonka kwenye mtandao wake wa X.
Wanaharakati kadhaa na mawakili ambao walifika makao hayo ya polisi walikatazwa kumwona wakili hiyo. Hilo lilisababisha waimbe nyimbo za kishujaa huku wakitaka wakili huyo aachiliwe huru.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Haki Afrika Yusuf Aboubakar alieleza Taifa Leo kuwa kikosi chake na kile cha Vocal Afrika kinachoongozwa na Hussein Khalid walizuiwa kumwona Bw Kebaso
“Hii si lolote si chochote ila ni serikali tu ndiyo inajaribu kuwatishia Wakenya wanaoikosoa. Bw Kebaso amekuwa akianika maovu serikalini kupitia miradi iliyokwama na hii imekasirisha baadhi ya watu,
“Kijana huyo anastahili kuruhusiwa awaone mawakili wake, azungumze nao na iwapo kuna kosa, ashtakiwe mahakamani,” akasema Bw Aboubakar.
Saa chache kabla ya kukamatwa kwake, Bw Kebaso ambaye amejitangza kiongozi wa Chama cha INJECT Kenya, aliweka video mitandaoni akishutumu vikali jinsi mwanaharakati mmoja wa Mombasa aliteswa na watu wanaodaiwa walikodishwa na maafisa wa ngazi ya juu katika gatuzi hilo.
Alitoa wito kwa vitengo vya usalama viharakishe uchunguzi na kumkamata Gavana Abdulswamad Nassir.
“Gavana anastahili kuchunguzwa na ashtakiwe. Kama hilo halitafanyika, niko tayari kusitisha shughuli na kuongoza maandamano ya kitaifa,” akasema.
Bado haijabainika iwapo kukamatwa kwa Bw Kebaso na kuzuiliwa kwake na polisi kunahusishwa na machapisho yake mitandaoni.