Habari za Kitaifa

Tuhuma za ubakaji wa bloga zinavyotishia jina la ‘Mwana Mwema’ la Abdulswamad Nassir

Na BRIAN OCHARO October 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma jana alikosa kumfungulia mashtaka Waziri wa Ardhi wa Kaunti ya Mombasa, Mohamed Hussein, aliyekuwa amekamatwa kwa madai ya kuhusika katika utekaji nyara na ulawiti wa mwanablogu.

Haya yalijiri huku Gavana Abdulswamad Nassir akithibitisha kuwa yeye na mamake, Bi Nassim Shariff Nassir, walikuwa wameitwa na polisi kurekodi taarifa kuhusu suala hilo hilo.

Polisi walidai mahakamani awali kwamba mwanablogu huyo alitekwa nyara na kulawitiwa baada ya kuweka video kwenye mtandao wa kijamii wa TikTok ambayo huenda ilimkasirisha Gavana Nassir na wafuasi wake.

Akizungumza katika makao makuu ya kaunti hiyo baada ya Bw Hussein kuachiliwa kutoka mikononi mwa polisi, gavana huyo alishikilia kuwa yuko tayari kuthibitisha kuwa hana hatia.

“Kwa jinsi ninavyomuonea huruma mtu huyo, familia yangu haitamsamehe tu bali itamwachia Mungu. Mama yangu amenyanyaswa na leo anatuhumiwa pamoja na mwanawe, natumai polisi watafanya hima kubaini ukweli wa suala hili,” alisema.

Kulingana na gavana huyo, suala hilo limeweka familia yake nzima katika hali ngumu. Alidai kuwa, nyumba zao zilivamiwa na watu wasiojulikana wakiwa na silaha ambao wamekuwa pia wakilifuata gari lake lakini hakuna hatua zinazochukuliwa licha ya kutoa taarifa kwa polisi. Hata hivyo, hakuonyesha wanahabari ithibati yoyote kuhusu hayo.

“Katika maisha yangu yote, si mimi mwenyewe wala mtu yeyote wa familia yangu ambaye amewahi kuvuka mpaka na kufanya tendo la aina yoyote ya unyanyasaji dhidi ya mtu yeyote,” alisema.

Gavana Abdulswamad Nassir akithibitisha Jumatatu kuwa yeye na mamake, Bi Nassim Shariff Nassir, walikuwa wameitwa na polisi kurekodi taarifa kuhusu kesi ya ubakaji. Picha|Kevin Odit

Bw Hussein iliachiliwa baada ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka kupewa amri ya Mahakama Kuu iliyokataza kukamatwa, kuzuiliwa na kuingiliwa kwa uhuru wake.

Bw Hussein alikuwa amekamatwa na maafisa kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) mnamo Jumapili. Agizo la kuzuia polisi kumkamata na kumzuilia Bw Hussein lilitolewa na Jaji wa Mahakama Kuu Wendy Kagendo, mnamo Septemba 23.

Aliidhinisha kesi hiyo kuwa ya dharura na kuamuru kwamba hati za mahakama zipelekwe kwa ODPP, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na DCI, ambao walikuwa wameorodheshwa kama washtakiwa.

Jaji huyo hata hivyo alifafanua kuwa, agizo hilo halikuzuia DCI kufanya uchunguzi kuhusiana na kutekwa nyara na kulawitiwa kwa mwanablogu huyo wa Mombasa.

Mnamo Septemba 27, jaji aliongeza muda wa maagizo ya kuwazuia polisi kumkamata, kuzuiliwa na kuingilia uhuru wa Bw Hussein.
Vilevile, aliwapa washtakiwa hadi jana, Septemba 30, kuwasilisha majibu yao.