Mshikemshike wanukia Bunge, Seneti wakitofautiana kuhusu dili nono za umeme
BUNGE la Kitaifa na lile la Seneti linaelekea kutofautiana kuhusu iwapo mikataba ya ununuzi wa umeme (PPAs) kutoka kwa kampuni za kibinafsi za kuzalisha kawi hiyo (IPPs) inafaa kuongezewa muda au mikataba mipya itiwe saini.
Seneti kupitia hoja itakayojadiliwa leo inaitaka serikali kutia saini mikataba mipya au kuongeza muda wa kutumika kwa mikataba ya sasa.
Lakini Bunge la Kitaifa linataka shughuli ya kutia saini mikataba ya ununuzi wa umeme kutoka kwa IPPs icheleweshwe, hadi uchunguzi unaoendeshwa na Kamati kuhusu Kawi ukamilishwe na ripoti iidhinishwe katika kikao cha wabunge wote.
Hoja ya Seneti iliyodhaminiwa na kamati yake kuhusu kawi – inayoongozwa na Seneta wa Nyeri Wamatinga Wahome – inajiri kwa misingi kwamba masharti yaliyowekewa Kampuni ya Kusambaza Umeme Nchini (KPLC) na Bunge la Kitaifa dhidi ya kutia saini mikataba mipya ya IPPs, yamekamilika.
Bunge la Kitaifa pia lilionya KPLC dhidi ya kuongeza muda wa matumizi ya mikataba ya sasa.
“Ili kuwakinga Wakenya dhidi ya bei ya juu ya umeme Seneti inaamua kuwa Wizara ya Kawi na KPLC ziruhusiwe kutia saini mikataba mipya ya ununuzi wa kawi na kampuni za kibinafsi za kuzalisha umeme au ziongeze muda wa mikataba ya sasa,” hoja hiyo inasema.
Hoja hiyo itajadiliwa kesho, siku chache baada ya Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi kufichua kwamba kuna uwezekano wa kutiwa saini kwa mikataba mipya ya ununuzi umeme.
Bw Wandayi alisema hatua hiyo itaruhusu kampuni za kibinafsi zinazozalisha umeme (IPPs) kuimarisha uzalishaji wa kawi yao, ambayo huwa ni ya kupiga jeki hifadhi ya kitaifa.
“Bila shaka tunaomba Bunge kuondoa marufuku hiyo ili kutoa nafasi kwa IPPs kuzalisha kawi nyingi na hivyo kuimarisha hifadhi ya kitaifa,” akaeleza Waziri.
Tangu Bw Wandayi aliingie ofisini Agosti 8, 2024 kumetokea visa viwili vya umeme kupotea kote nchini. Hali hiyo imesababishwa na hitilafu katika nyaya za kusambaza umeme wenye nguvu nyingi.
“Dalili za kutokea kwa hali hii zimekuwepo kwa muda mrefu, hali inayochangiwa na uwekezaji finyu katika miradi ya kuimarisha miundo msingi,” Waziri alieleza baada ya tukio la hivi punde la umeme kupotea kote nchini mnamo Agosti 30, 2024.
Hoja ya Seneti pia inaitaka Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Mafuta (EPRA) kuharakisha mchakato wa kutoa leseni hitajika kwa kampuni za IPPs ili zianzishe viwanda vipya vya kuzalisha kawi.
KPLC husambaza umeme kwa wateja zaidi ya 9.6 milioni na hununua asilimia 17 ya umeme huo kutoka mataifa jirani. Hitaji la umeme linazidi kuongezeka nchini ilhali mchakato wa kuanzishwa kwa viwanda vipya vya uzalishaji kawi hiyo unaendeshwa kwa mwendo wa kinyonga.
Mwaka mmoja na nusu uliopita, visa vya kupotea kwa umeme vimeathiri hata uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).
Hoja ya Seneti pia inaitaka Mamlaka ya Kusimamia Kawi na Mafuta (EPRA) kuharakisha mchakato wa kuziwezesha kampuni za IPPs kupata leseni hitajika ili kuanzisha viwanda vipya vya kuzalisha kawi.
Kampuni ya KPLC, ambayo husambaza umeme kwa zaidi ya wateja milioni 9.6 hununua asilimia 17 ya umeme kutoka mataifa jirani.
Kampuni hii inakabiliwa na changamoto kwa sababu hitaji la umeme linaongezeka ilhali mchakato wa kuanzishwa kwa viwanda vipya vya kuzalisha kawi unaendeshwa kwa mwendo wa kinyonga.