Ruto azidi kunyamaza wandani wakimtia naibu wake makucha
Gumzo ya kumbandua Bw Gachagua lilibainika kuwa si mzaha tena wakati Spika Moses Wetang’ula alipotangaza kupokea mswada huo na kusema kwamba umefikisha vigezo vyote vya kujadiliwa na Bunge.
Hoja ya kumtimua ambayo iliwasilishwa Jumanne katika Bunge la Kitaifa na Mbunge wa Kibwezi Mashariki Mwengi Mutuse inataja matamshi ya kibaguzi na kumdharau rais miongoni mwa mengine 10 kama baadhi ya sababu za kutaka atimuliwe ofisini.
“Siku tofauti katika hafla tofauti, Mheshimiwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alitamka maneno ya kutenga na kunyima, kinyume cha sheria, baadhi ya watu wa Kenya na maeneo ya nchi nafasi sawa za uteuzi katika utumishi wa umma na rasimali za umma,” inasema hoja hiyo.
Bw Gachagua alitoa matamshi hayo akiwa katika hafla ya umma kaunti ya Kajiado akiashiria kuwa, miradi ya maendeleo ya serikali na kazi katika sekta ya umma zinapaswa kutengewa watu kutoka baadhi ya maeneo.
“Serikali ni kama kampuni, kuna hisa. Kuna wale waliowekeza hisa, kuna wale wameweka kidogo, kuna wale wamekataa, lakini wote ni Wakenya. Kwa hivyo ndio tukasema, kama wewe umeenda kupanda mahindi, ama wacha nipeane mfano wa ng’ombe kwasababu niko Kajiado. Wewe uko na ng’ombe yako ya maziwa, hiyo ng’ombe imezaliwa ikiwa ndama, umeichunga vizuri, umepatia majani, umenunulia lishe, umepatia chumvi, umepeleka kwa malisho, umepatia maji, imezaa, imeanza kukamuliwa. Wewe unatakiwa kwanza uwe mtu wa kwanza kukamua hiyo ng’ombe na kunywa maziwa,” Bw Gachagua alisema wakati huo.
Kulingana na waandalizi wa mashtaka dhidi ya Bw Gachagua, katika matamshi hayo ya naibu rais yalikuwa ya kuzua mgawanyiko na uchochezi wanaodai alisisitiza kwa kusema: “Haiwezekani mtu ambaye alikua anakupigia kelele ukichunga hii ng’ombe, na kusema hii ng’ombe ni ile ya kienyeji hakuna haja ya kushugulika naye, hii ng’ombe ni bure haiwezi kutoa maziwa, hii ng’ombe hata iko na jicho moja, wachana nayo unapoteza wakati. Saa ile ng’ombe imezaa imetoa maziwa…amekuja na kikombe, amekuja na sufuria, anataka atolewe maziwa. Mimi nikasema hiyo haiwezekani. Nikasema yule mwenye hii ng’ombe na kuichunga na kuitunza, kwanza akamue maziwa, yeye na watoto wake wakunywe, ile itabaki aitie majirani. Ata yule alikuwa anapiga kelele akisema hii ng’ombe ni bure na haiwezekani kama kunayo imebaki pia apewe, kama hakuna imebaki atembee. Si hiyo namna hiyo?”
Waandalizi wa mashtaka wanasema kwamba, Bw Gachagua alirudia matamshi hayo katika hafla tofauti maeneo mbali mbali nchini.
Wanamshtaki pia kwa ukiukaji wa katiba wakidai amekuwa akitelekeza majukumu yake kama naibu rais ya kumsaidia kiongozi wa nchi “ kwa kutoa matamshi yanayotofautiana na sera za pamoja za serikali.
Inadaiwa kuwa, Bw Gachagua alitenda kosa hilo kwa kutetea watu ambao serikali iliagiza wafurushwe kutoka kingo za mito kaunti ya Nairobi.
“Mnamo Aprili 30 2024 Mheshimiwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alitoa matamshi kinzani na uamuzi wa pamoja wa Baraza la Mawaziri wa kuhamisha watu kutoka kingo za mito ya Nairobi.
Aidha, analaumiwa kwa kutofautiana na Rais kwamba hakuna raia anayepaswa kubaguliwa katika utoaji wa huduma za serikali.
Kauli za Naibu Rais zinahujumu utekelezaji wa majukumu ya serikali ya kitaifa na ukiukaji wa maamuzi ya pamoja ya Baraza la Mawaziri na ni sawa na kumdharau rais, jambo ambalo ni kinyume na katiba ya Kenya,” yanasema mashtaka dhidi ya Gachagua.
Bw Gachagua pia anashtakiwa kwa kuvuruga ugatuzi kwa kuingilia usimamizi wa serikali ya kaunti ya Nairobi kwa kupinga kuhamishwa kwa wafanyabiashara kutoka kati kati ya jiji.
Bw Gachagua amekuwa akipinga kuhamishwa kwa wafanyabiashara kutoka soko la Marikiti hadi soko la barabara ya Kangundo.
Vile vile, vita vyake dhidi ya pombe haramu vimerudi kumsumbua vikitajwa miongoni mwa mashtaka ya kumuondoa ofisini.
“Mheshimiwa Naibu Rais Rigathi Gachagua alitwaa majukumu ya kikatiba ya serikali za kaunti,” wanasema.
Bw Gachagua pia anakabiliwa na tuhuma za uhalifu wa kiuchumi na matumizi mabaya ya ofisi ambapo anadaiwa kujilimbikizia mali isiyoelezeka ndani ya miaka miwili iliyopita, zikiwemo hoteli na ardhi.
Anadaiwa kushindwa kuheshimu na kutetea Katiba, huku matamshi yake ya uchochezi yakidaiwa kukiuka Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa kwa kuendeleza chuki za kikabila.
“Vitendo vyake vinaonyesha kudharau kwa wazi Katiba ambayo ameapa kuilinda, na kuweka maadili yetu ya kidemokrasia hatarini,” Mwengi alisema.
Hoja hiyo pia inadai Gachagua alijihusisha na matumizi mabaya ya afisi, na kukiuka sheria za kupambana na ufisadi.
“Kujihusisha na ufisadi na ulanguzi wa fedha ukiwa ofisini kunadhoofisha imani ya umma na kukiuka sheria za kupambana na ufisadi,” Mwengi alisema.
Zaidi ya hayo, Bw Gachagua anatuhumiwa kwa madai ya kutoa taarifa za uongo na kukiuka Sheria ya Uongozi na Uadilifu.
Mwisho, hoja hiyo inataja utovu wa nidhamu uliokithiri, ikiwa ni pamoja na mashambulizi dhidi ya Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi, kutotii Rais, kuwatisha maafisa wa umma, na kushawishi vitendo vya ufisadi.
Taarifa ya Benson Matheka, Collins Omulo na David Mwere