Kimataifa

Iran yanyeshea Israel makombora kulipiza kisasi kwa mauaji ya kiongozi wa Hezbollah Nasrallah

Na REUTERS October 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

JERUSALEM, ISRAEL

IRAN imeishambulia Israel kwa makombora 180, jambo ambalo linaaminiwa litapepeta mzozo kati ya Israel na makundi yanayoungwa mkono na Iran ya Hamas na Hezbollah.

Msemaji wa jeshi la Israel, Daniel Hagari, amesema shambulio hilo la makombora lililofanywa na Iran Jumanne lilinuia kuwaua maalfu ya raia wa Israel na halikuwa la kawaida na wala halikutarajiwa.

Jeshi la Israel pia limelilaani shambulio hilo likilirejelea kuwa la hatari la kupepeta machafuko.

Hagari amesema Iran na washirika wake wanataka kuiangamiza Israel kama njia ya kulipiza kisasi kwa mashambulizi Lebanon yaliyopelekea kuua Kiongozi wa Hezbollah, Hassan Nasrallah.

Naye Rais wa Amerika, Joe Biden amesema nchi yake inaiunga mkono kikamilifu Israel na inaitaka ijibu shambulio hilo la Iran la makombora ya masafa marefu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika ikulu yake mjini Washington, Biden amesema kuna mazungumzo yanayoendelea kuhusu jinsi Israel itakavyojibu shambulio la Iran na kwamba athari zake zitaonekana.

Biden amesema atazungumza na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

Wakati huo huo, Urusi inasema sera ya Amerika kuhusu Mashariki ya Kati imeshindwa kabisa kuzaa matunda.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Urusi Maria Zakharova amesema katika taarifa yake aliyoiandika kwenye mtandao wa Telegram kwamba utawala wa rais Biden umefeli kabisa na imeshindwa kudhibiti mapigano hayo.

Kando na hayo, alisema kuwa Amerika haina mpango wowote wa kudhibiti mapigano hayo.

Naye Wizara ya mambo ya nje ya Iran imelitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lichukue hatua za haraka kuepusha vitisho dhidi ya amani na usalama wa Mashariki ya Kati.

Baraza la usalama jana lilifanya kikao cha dharura kujadili ongezeko la machafuko Mashariki ya Kati.

Msemaji wa ofisi ya balozi wa Uswiwi katika Umoja wa Mataifa, alisema mkutano huo ulifanyika saa nne asubuhi saa za New York.

Umoja wa Ulaya umetoa wito mapigano yasitishwe mara moja Mashariki ya Kati.

Mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo, Josep Borell ametumia maneno makali kulikosoa shambulio la Iran dhidi ya Israel akisema kuwa shambulio hilo limefungua ukurasa wa mashambulio ya mara kwa mara kati ya nchi hizo mbili akiongeza kuwa Umoja wa Ulaya umejitolea kikamilifu na kwa dhati kudhibiti vita vya kikanda.

Wakati haya yakiendelea, Lebanon imefungua tena safari za anga kufuatia shambulio la Iran nchini Israel.

Waziri wa usafiri wa Lebanon Ali Hamieh amesema baada ya kufuatilia kwa ukaribu jinsi hali ilivyo na kutokana na pendekezo la wataalamu mbalimbali, wameamua kufungua tena safari hizo.