Habari Mseto

Madiwani wakataa kumsamehe Mutai, wamtimua mamlakani licha ya agizo la korti

Na VITALIS KIMUTAI October 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

GAVANA wa Kericho, Erick Mutai, Jumatano alitimuliwa mamlakani baada ya madiwani 31 miongoni mwa 47 kuunga hoja ya kumuondoa licha ya amri ya korti iliyozima Bunge la Kaunti kuendelea na mchakato huo.

Madiwani 16 ambao ni wandani wa mkuu huyo wa kaunti walisusia kikao hicho wakipinga uhalali wa mchakato wa kumtimua.

Katika hoja iliyowasilishwa na MCA wa Wadi ya Sigowet, Kiprotich Rogony, Gavana alishutumiwa kwa kukiuka katiba, matumizi mabaya ya afisi na kukosa nidhamu.

Licha ya madai mazito yaliyomkabili, Bw Mutai aliamua kutofika mbele ya bunge la kaunti kujitetea na badala yake akatuma timu yake ya mawakili wakiwemo Katwa Kigen na Manase Tunen kumwakilisha.

Mchakato wa kumng’oa mamlakani uliendelea licha ya agizo la mahakama lililotolewa na Jaji Joseph Sergon mnamo Jumanne, liliozuia bunge la kaunti hiyo kujadili wala kupigia kura hoja ya kumtiimua hadi kesi iliyowasilishwa na Gavana itakaposikizwa na uamuzi kutolewa.

Spika Patrick Mutai alisisitiza kura 31 inatosha kufikisha kiwango kinachohitajika kisheria kumtimua Gavana Mutai lakini madiwani 16 wanaomuunga mkono Gavana walihoji kwamba idadi sahihi inastahili kuwa 32 miongoni mwa madiwani 47.

“Kulingana na rekodi katika bunge la kaunti, madiwani 31 waliokuwepo wamepiga kura kuunga mkono hoja hiyo. Hoja imepitishwa na Gavana Mutai ametimuliwa na Bunge la Kaunti ya Kericho,” alisema Spika Mutai.

Madiwani ambao ni wandani wa Gavana akiwemo Diwani wa Wadi ya Kapsoit Paul Tarimbo Chirchir na Diwani wa Wadi ya Chaik, Korir, walipinga wakisema mchakato ulikosa kutimiza kiwango kinachohitajika kisheria kwa kukosa kura moja.