Habari za Kitaifa

Gachagua akitimuliwa sahau kabisa Mlima Kenya, wazee waambia Ruto

Na MERCY MWENDE, STEPHEN MUNYIRI October 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BARAZA wa Wazee wa jamii za eneo la Mlima Kenya limetishia kutomuunga mkono tena Rais William Ruto ikiwa naibu wake Rigathi Gachagua ataondolewa mamlakani.

Akiongea baada ya mkutano wa baraza hilo mjini Nyeri, mwenyekiti wa vuguvugu la Amani kwa Wote Kenya, Bw Paul Mwiti Kariuki, ambaye pia ni mwenyekiti wa wazee hao, alisema hatima ya Dkt Ruto na Gachagua imeshikana na wanapaswa kuondoka mamlakani wakati mmoja.

“Kumuondoa afisini Naibu Rais kunamaanisha kuwa unaondoa eneo la Mlima Kenya kutoka uongozini na akienda nyumbani sidhani kuwa kama eneo tutakubali uongozi wa Rais Ruto. Ikiwa Rigathi anaenda nyumbani, basi waende wote wawili,” akasema.

Bw Kariuki alikariri kuwa eneo la Mlima Kenya lilichangia pakubwa ushindi wa Dkt Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2022 akisema wakazi wa eneo hilo walimpigia kura kwa sababu alishirikiana na Gachagua.

Alisema jaribio lolote la kumwondoa afisini ni sawa na kulichokoza eneo la Mlima Kenya.

Bw Kariuki alieleza kuwa baraza hilo limegadhabishwa na misukosuko ya kisiasa inayoshuhudiwa nchini akielezea kujitolea kwake kulinda wadhifa wa Naibu Rais hadi atakapokamilisha muhula wake.

Wakati wa mkutano huo, wazee hao pia walitangaza maombi maalum ya kijamii yatakayofanyika katika uwanja wa Ruring’u mnamo Oktoba 25, 2024.

Viongozi watatumia fursa hiyo kuombea amani, umoja na uthabiti wakilenga changamoto zinazokabili jamii ya GEMA.

Pius Njogu ambaye ni Katibu Mkuu wa Muungano wa Mashujaa wa Mau Mau alielezea kutamaushwa kwake na vita vya kisiasa vinavyoshuhudiwa ndani ya muungano wa Kenya Kwanza.

“Tulishiriki uchaguzi na tukahakikisha kuwa Ruto ameshinda. Lakini inavunja moyo kusikia kuwa mtu wetu ambaye alituhimiza kujitokeza kupiga kura anaondolewa afisini. Hatuamini hii,” Njogu akalalamika.

Wazee hao walisema hayo huku wakazi wa eneo bunge la Mathira, anakotoka Gachagua, wakikusanyika mjini Karatina kumwombea Naibu Rais.

Maombi hayo yaliendelea huku taharuki ikitanda mjini humo baada ya polisi wa kupambana na fujo kuletwa saa chache baada ya hoja hiyo kuwasilishwa katika Bunge la Kitaifa.

Maombi hayo yaliongozwa na Askofu Evans Njoroge wa Kanisa la Faith Manifestation ambaye aliomba Mungu aingilie kati ili Bw Gachagua anusurike kuondolewa afisini kupitia hoja hiyo.

Askofu Njoroge aliomba kwamba Rais Ruto na naibu wake “wapige magoti wasuluhishe tofauti zao kupitia maombi” akisema kanisa limevunjwa moyo na yale yanayoshuhudiwa nchini.

“Nasikia kuna watu wanataka kumwondoa afisini Naibu Rais, hatukutarajia mambo yageuke hivi. Nawaomba wawili hao wapige magoti na watafute ushauri kutoka kwa Mungu ili wasalie pamoja na waifanyie nchi hii kazi,” akasema.

Maombi hayo yalifanyika katika soko la wazi la Karatina japo hayakuhudhuriwa na watu wengi.

Ni madiwani watatu pekee kati ya madiwani saba kutoka eneo bunge la Mathira waliohudhuria maombi hayo.

Viongozi hao walisema wanaounga mkono hoja ya kumuondoa afisini Bw Gachagua wanaongozwa na “nia mbaya”.