Mlo wa matumbo ni hatari, waweza kukusababishia maradhi ya moyo, Wataalamu waonya
IDADI ya walaji matumbo imeongeza ndani ya miaka michache iliyopita, licha ya wataalamu wa lishe kuonya kwamba ulaji wake unasababisha unene kupita kiasi na maradhi ya moyo.
Vile vile, imebainika kuwa matumbo hayana utajiri mkubwa wa madini ikilinganishwa na aina zingine za nyama.
Wengi wa wauzaji matumbo wanasema hali ngumu ya kiuchumi inayoathiri familia nyingi ndio imechangia watu wengi kukimbilia aina hii ya nyama.
Data kutoka kwa ripoti ya hivi punde ya uchunguzi wa hali ya kiuchumi inaonyesha kuwa, tani 74 ya matumbo zililiwa nchini katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023.
Danson Wanderi, 42, muuzaji nyama katika mtaa wa Kibera, Nairobi anasema idadi kubwa ya wateja katika bucha yake hununua matumbo.
“Ndani ya muda wa miezi michache iliyopita, nimeshuhudiwa ongezeko la mauzo ya matumbo,” anasema mfanyabiashara huyo ambaye bucha yake iko karibu na baa.
“Kwa wastani, mimi huuza kilo 25 kila siku, hivyo huuza kilo 160 kwa wiki. Kila jioni matumbo huwa yameisha na hivyo mimi huagiza nyingine kutoka kichinjio cha karibu kila siku,” anaeleza Bw Wanderi.
Bei ya chini zaidi ya matumbo ni Sh300 kwa kilo ikilinganishwa na nyama halisi ambayo huuzwa kuanza Sh760 hadi Sh1,200 kulingana na thamani. Hii ina maana kuwa matumbo hugharimu pesa kidogo na hivyo huvutia wanunuzi wengi.
Japo ulaji wa matumbo umeongezeka, wataalamu wa lishe wanaonya kuwa ulaji kupindukia unahusishwa na madhara ya kiafya.
Kepha Nyanumba, mtaalamu wa lishe katika kaunti ya Nairobi anaeleza kuwa japo bei ya matumbo ni nafuu, hayana madini bora kwa mwili.
“Matumbo ni mojawapo ya chakula chenye protini lakini yenye thamani ya chini, ikilinganishwa na protini kutoka kwa nyama ya kawaida, samaki au viumbe wengine wa majini. Matumbo hayana aina ya madini yenye manufaa ya kuimarisha hali ya ngozi na mifupa,” akasema, akiongeza kuwa watu wasile matumbo kwa wingi.
“Matumbo yanasheheni kiasi kikubwa cha mafuta ambayo ni hatari kwa watu wanaougua maradhi ya moyo na kiharusi,” anaeleza Nyanumba.
Bw Nyanumba pia anasema kuwa matumbo yana kiwango cha juu cha mafuta yasiyoweza kuyeyuka, ambayo huongeza uzani na hatari ya magonjwa kama vile kisukari na shinikizo la damu.
“Vile vile, matumbo yako na sumu inayoweza kusababisha ongezeko la asidi mwilini na hivyo kusababisha magonjwa ya kuvimba miguu,” anaeleza.
Matumbo pia huchukua muda mrefu kusagwa, hali inayosababisha matatizo ya kwenye utumbo wa mwanadamu.