Ajabu kaunti kulalamikia kukosa hela akaunti ikiwa imejaa mabilioni
KAUNTI zina zaidi ya Sh42 bilioni katika akaunti yao licha ya baadhi ya kaunti kukabiliwa na tishio la shughuli zake kulemazwa, Waziri wa Fedha John Mbadi amefichua.
Waziri alieleza maseneta kwamba Hazina ya Mapato ya Kaunti (CRF) inashikilia kiasi cha hadi Sh42.38 bilioni ambazo bado hazijatwaliwa na kaunti.
Haya yalijiri huku Waziri akisema Hazina Kuu wiki iliyopita, ilitoa Sh31.8 bilioni kwa kaunti kama mgao wa mapato kwa Julai 2024.
Aidha, alisema Hazina Kuu ilisambaza Sh30.8 bilioni kama mgao wa kaunti kwa bajeti iliyokamilika Juni 30, 2024.
Akihutubia Seneti Jumatano, Waziri Mbadi alifafanua kuwa fedha hizo ambazo zimekaa tu bila kutumika zinajumuisha Sh3 bilioni zilizopangiwa kwa matumizi ya kila siku na Sh969 milioni chini ya kura ya maendeleo.
“Tunapozungumza sasa, kuna Sh42.38 bilioni ambazo hazijajumuishwa au kutwaliwa na kaunti ambazo zimekaa tu CRF. Hela zipo kwenye akaunti. Pesa hizo zinapowekwa katika akaunti ya CRF, zinapaswa kulipa mishahara na matumizi mengineyo ya maendeleo,” alisema Bw Mbadi.
“Tunahitaji kuwa na mchakato laini wa kukusanya na kutumia pesa kwa sababu hatutaki hali ambapo malimbikizi ya hela yanalundikana kwenye akaunti zisizotumiwa kwa sababu haziongezi thamani kwa uchumi wetu na zinapunguza kasi ya ukuaji kiuchumi,” alisema.
Alitoa wito kwa wakuu wa kaunti kulainisha mambo na Mdhibiti wa Bajeti ili kuhakikisha mabilioni ya hela hazikai tu kwenye akaunti pasipo kutumika.
“Kama watu waliotwikwa jukumu la kuangazia kaunti, mnapaswa kushinikiza kaunti kutatua masuala yake na Mdhibiti wa Bajeti ili tusiwe na mlundikano wa hela katika akaunti za CRF,” alieleza maseneta.
Ajabu ni kuwa, magavana walikuwa wameonya kwamba wangelemaza serikali za kaunti kutokana na hali ya ukosefu wa hela iliyosababishwa na kuchelewesha kutoa fedha kwa kaunti hivyo kutishia shughuli zao.
Akijibu kuhusu suala la kuchelewesha usambazaji wa fedha za kaunti, Mbadi alifichua kuwa Hazina Kuu, wiki iliyopita ilitoa Sh31.8 bilioni kwa kaunti kama mgao wa Jula licha ya bunge kuchelewa kupitisha sheria za kuwezesha shughuli hiyo.
Hatua hiyo, alisema, ilifuatia agizo la Mwanasheria Mkuu, Dorcas Oduor, la kuwezesha kuachilia asilimia 50 ya fedha hizo kwa kaunti kulingana na mgao wa bajeti yam waka uliopita wa Sh385 bilioni.
Alisema matatizo yaliyojitokeza mwanzoni mwa bajeti mpya kuhusu kutoa pesa ni ya kisheria hivyo alilazimika kuomba ushauri wa mwanasheria mkuu.