Habari Mseto

Polisi wafyatua vitoa machozi kutawanya vijana waliong’ang’ania kazi ya kuchimbua Mto Ngong

Na SAMMY KIMATU October 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

ILIWALAZIMU maafisa wa polisi wa kupambana na ghasia na wenzao wanaovalia kiraia kufyatua vitoa machozi kuwatawanya vijana waliokuwa na gadhabu wakiandamana kulalamika majina yao kutokuwepo katika orodha ya vijana wanaofanya kazi kukomboa kingo za Mto Ngong.

Haikuwa shughuli kama kawaida katika mtaa wa mabanda wa Mukuru-Hazina na katika eneo la Kambi Moto huku vijana wakiwafukuza wenzao waliokuwa wakifanya kazi katika Mto Ngong.

Kamanda wa polisi eneo la Makadara, Bi Judith Nyongesa aliambia Taifa Leo kwamba katika kukurukakara hizo, ilibidi maafisa wake wakiongozwa na afisa mkuu wa kituo cha polisi cha Hazina, Bw Robert Mbui kutumwa ili kutuliza hali.

Ilikuwa ni patashika na mguu niponye karibu na daraja la Hazina/Kayaba ambapo vitoa machozi viliathiri akina mama na watoto waliokuwa mitaani.

Vijana wakiendelea na kazi ya kuchimbua taka zilizomwagwa Mto Ngong. Picha|Sammy Kimatu

Vilevile, masomo yalivurugwa katika shule ya Kenya Kids Learning Centre ambako masomo yalikuwa yakiendelea.

Hata hivyo, Jumatano, naibu kamishna wa Starehe, Bw John Kisang alizuru katika afisi za mkuu wa tarafa South B ili kutathmini malalamishi kuhusu majina ya vijana ambao walifanya kazi Jumanne na Jumatatu asubuhi kuamkia kukuta majina yao hayamo katika orodha ya waliopangiwa kufanya kazi Alhamisi.

Baadaye, shughuli zilianza rasmi za kusafisha kingo za mto mbapo vijana hao waligawanywa katika makundi manne.

“Leo tunakusanya takataka zilizotupwa na wakazi katika kingo za mto kisha baadaye zizolewe na kupelekwa kunakostahili,” dada ambaye aliomba kutotajwa joina lake akahoji.

Kumekuwa na malalamishi kutoka kwa baadhi ya wakazi mitaa ya Mukuru kuhusu mchakato mzima wa kusajili vijana hao huku wakidai wengine waliopewa kazi hawawezi kuingia ndani ya Mto Ngong kutokana na umri huku tetesi zikiarifu wanahabari kulikuwa na madai ya ufisadi japo madai hayo yangali bado hayajathibitishwa na idara husika za serikali.