Dimba

Real, Atletico na Bayern waona usiku mrefu Uefa

October 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NYON, Uswisi

Miamba Real Madrid, Bayern Munich na Atletico Madrid waliona usiku mrefu viwanjani baada ya kufunzwa soka na wanyonge kwenye Klabu Bingwa Ulaya, Jumatano.

Mabingwa mara 15 Real, ambao pia wanatetea taji, walipigwa bao moja chungu na wenyeji Lille kupitia penalti safi kutoka kwa mshambulizi Jonathan David kabla ya mapumziko. Kiungo mkabaji Eduardo Camavinga alinawa mpira ndani ya kisanduku chake. Masupastaa Kylian Mbappe na Luca Modric walianza mpepetano huo kutoka kwenye benchi.

Ni mara ya kwanza tangu Novemba 2016 vijana wa kocha Carlo Ancelotti walishindwa kuzoa ushindi katika mechi tatu mfululizo za ugenini kwenye Klabu Bingwa Ulaya.

Pia, ni kichapo cha kwanza cha Real kwenye mashindano haya ya kiwango cha juu kabisa ya klabu za Bara Ulaya tangu walimwe 4-0 na Manchester City mwezi Mei 2023 na cha kwanza katika mechi za makundi tangu Oktoba 2022 waliponyukwa na Leipzig 3-2.

Atletico walibomolewa 4-0 na Benfica mjini Lisbon nchini Ureno. Benfica walipata mabao kupitia kwa Muhammed Kerem, Angel Di Maria (penalti), Alexander Bah na Orkun Kokcu (penalti).

Ni kipigo kikali kabisa ambacho vijana wa kocha Diego Simeone wamepata kwenye Klabu Bingwa Ulaya mikononi mwa timu yoyote inayotoka Ureno.

Bayern ya kocha Vincent Kompany ilisalimu amri ya Aston Villa baada ya mshambulizi Jhon Duran kukamilisha pasi safi kutoka kwa beki Pau Torres kwa kumwaga kipa Manuel Neuer dakika ya 79 ugani Villa Park. Ushindi huo ulimaliza rekodi ya Bayern kutopoteza katika mechi 41 katika makundi ya Klabu Bingwa Ulaya.

Ulikuwa ushindi wa kihistoria kwani Villa sasa imekuwa timu ya pili tu kutoka Uingereza kushinda mechi mbili za kwanza za Klabu Bingwa Ulaya tangu msimu 1992-1993 baada ya Leicester msimu 2016-2017.

Kipa Emiliano Martinez pia alikuwa shujaa wa Villa baada ya kupangua makombora hatari kutoka kwa Serge Gnabry, Mathys Tel na Harry Kane.

Liverpool walihakikisha timu kutoka Uingereza zinakamilisha raundi hiyo ya mechi kwa ushindi baada ya kupapura Bologna 2-0 kupitia mabao ya Alexis Mac Allister na Mohamed Salah ugani Anfield.

Matokeo hayo yalifanya Arne Slot kuwa kocha wa kwanza wa Liverpool kutwaa ushindi mara nane katika mechi zake tisa za kwanza.

Naye, Salah ni mchezaji wa kwanza wa Reds kupachika goli katika michuano mitano mfululizo ya nyumbani katika Klabu Bingwa Ulaya.

Matokeo (Oktoba 2):

Shakhtar Donetsk 0-3 Atalanta, Girona 2-3 Feyenoord, Benfica 4-0 Atletico Madrid, Liverpool 2-0 Bologna, Leipzig 2-3 Juventus, Lille 1-0 Real Madrid, Sturm Graz 0-1 Club Brugge, Aston Villa 1-0 Bayern Munich, Dinamo Zagreb 2-2 Monaco.