Habari za Kitaifa

Kesi 11 za kumnusuru Gachagua mahakamani zagonga mwamba maoni yakikusanywa Ijumaa

Na SAM KIPLAGAT October 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Rais Rigathi Gachagua amefika kortini katika jaribio la kumi na moja la kutaka kusitisha mchakato wa kumuondoa mamlakani akidai kuwa madai dhidi yake ni ya uwongo mtupu.

Bw Gachagua alisema katika ombi hilo kwamba hoja ya kutaka kumtimua ilitokana na udanganyifu, upotoshaji wa ukweli wa mambo ambayo yamekuwa yakienezwa kwa umma ili kufikia malengo yasiyofaa yaliyo kinyume na katiba.

Aidha, Naibu Rais alisema mchakato wa siku moja wa ushirikishaji wa umma ambao ulianzishwa na Bunge hautoshi “kubatilisha uamuzi wa watu” ambao walimpigia kura yeye na Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu uliopita.

Bw Gachagua alitaja mchakato huo kuwa “uchochezi wa kisiasa uliopangwa dhidi ya uamuzi wa watu wa Kenya” na unanuiwa kukatiza mapema kazi yake kama mtumishi wa umma.

“Kwamba kwa kuzingatia sababu zilizotajwa hapo juu zikichunguzwa dhidi ya madhara makubwa sana ambayo yanaweza kumpata mlalamishi, itakuwa ni dhuluma kwa washtakiwa kuendelea na zoezi la kumtimua ofisini mlalamishi ambalo matokeo yake ni kubatilisha uamuzi wa wapiga kura waliomchagua,” Bw Gachagua alisema kwenye kesi yake.

Alisema matokeo yasiyoweza kurekebishwa hoja ya kumtimua ikifanikiwa, ni kwamba atazuiliwa kabisa kushikilia wadhifa wowote wa umma.

Miongoni mwa mambo ambayo ameibua katika kesi ni madai kwamba amejilimbikizia mali inayokadiriwa kufikia Sh5.2 bilioni, akisema hayana msingi wowote.

“Iwapo mwasilishaji wa hoja angejisumbua kuniuliza au kufanya uchunguzi wa kimsingi kwenye rekodi za serikali kabla ya kutoa tuhuma zake za uwongo, za kishenzi, za kijeuri na mbovu, angepata ukweli,” alisema.

Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse alidai kuwa Bw Gachachua alinunua Hoteli za Outspan, Treetops Lodge, Olive Gardens Hotel, Vipingo Beach Hotel, Queens Gate Serviced Apartments na ardhi katika kaunti za Nyeri na Meru.

Bw Gachagua, hata hivyo, alisema kuwa hoteli ya Outspan ilinunuliwa kupitia mkopo wa benki na akashikilia kuwa amekuwa wazi kwa umma kuhusu umiliki wa hoteli hiyo kwani hakuna cha kuficha na mali hiyo si mali ya umma.

Alifafanua zaidi kuwa hoteli ya Treetops Lodge imekodishwa kutoka kwa shirika la kibinafsi.

“Similiki Hoteli ya Olive Gardens au Queens Gate Serviced Apartments. Mali hizi zilikuwa za marehemu kaka yangu, Nderitu Gachagua ambaye aliniteua kuwa msimamizi mwenza wa wosia wake,” akasema akiongeza kuwa mali hizo zinasimamiwa kwa mujibu wa matakwa yaliyotolewa katika wosia wake.

Bw Gachagua pia alikanusha madai kuwa anamiliki Vipingo Resort na kusema mali hiyo ni ya marehemu kakake Nderitu Gachagua, ambaye alimteua kuwa mtekelezaji mwenza wa wosia wake.

Amemkashifu Bw Mutuse akisema hakuna ripoti aliyoambatisha kuhusiana na mali yoyote iliyoorodheshwa ili kuonyesha thamani ya mali hizo.

Katibu wa Bunge alichapisha notisi ya kuwaalika wananchi kushiriki katika shughuli hiyo mnamo Ijumaa, Oktoba 4.Bw Gachagua alisema Wakenya katika nchi nzima wamepewa notisi ya siku moja kwa zoezi hilo ambalo linakiuka wazi kanuni za ushirikishaji wa umma.

Kesi yake ilikuwa ya pili kuwasilishwa jana na ya kumi katika juhudi za kusitisha mchakato wa kutimuliwa kwake kama naibu rais wa Kenya.

Kesi ya tisa iliwasilishwa na Victor Okoth na kuidhinishwa na Jaji Bahati Mwamuye kuwa ya dharura.

Jaji alikataa kutoa agizo la kusimamisha mchakato huo na badala yake akatenga isikilizwe Oktoba 10.

Kuna kesi zingine nane zilizowasilishwa na washirika wake na mashirika ya kutetea haki kutaka kumuokoa Gachagua.

Kesi hizo zimewasilishwa na Bw Cleophas Malala, Bw Obuli Namweya na watu wengine wawili, Hezron Okirgit, Caroline Wambui Mwangi, Jeremiah Gitari na Sheria Mtaani na Shadrack Wambui, zote katika mahakama kuu, Nairobi.

Kuna kesi kama hizo katika Mahakama ya Kerugoya na Nyahururu.