Mfumo wa ufadhili Elimu ya Juu usimamishwe na usubiri kesi, yaagiza mahakama
MAHAKAMA Kuu imesitisha muundo mpya wa ufadhili wa elimu katika vyuo vikuu baada ya mashirika matatu kuupinga yakidai ni kinyume cha katiba.
Jaji Chacha Mwita aliagiza Wizara ya Elimu isitishe muundo huo mpya wa ufadhili wa elimu ya juu kusubiri uamuzi wa kesi hiyo. Ni mfumo ambao umezua mkanganyiko katika taasisi za elimu ya juu.
Mashirika hayo yanayojumuisha Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya (KHRC), Elimu Bora na Kundi la Wanafunzi yalidai kuwa utekelezaji wa muundo huo umehamisha jukumu la kutoa elimu kutoka kwa serikali hadi kwa wazazi, ambao wengi wao wanatatizika kugharimia elimu ya watoto wao shuleni.
Zaidi ya hayo, walalamishi walisema hakuna uwazi kuhusu vyuo vikuu vilivyochaguliwa na kozi za kiufundi na wanafunzi wanatatizika kutokana na ukosefu wa maagizo ya wazi kutoka kwa Huduma ya Kutenga Nafasi katika Vyuo Vikuu Kenya (KUCCPS).
“Agizo linatolewa kuzuia washtakiwa, maajenti na wafanyakazi wao kutekeleza muundo mpya wa ufadhili wa elimu, kusubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa kesi,” Jaji Mwita alisema
Jaji aliagiza kesi hiyo isikizwe Desemba 16.
Muundo huo ulianzishwa kufuatia pendekezo la Jopokazi la Rais kuhusu Mageuzi ya Elimu.Walalamishi hao wanadai kuwa muundo huo ulitekelezwa kwa haraka bila mashauriano na bila sheria za kuuwezesha.
Mashirika hayo yalieleza kuwa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na Hazina ya Vyuo Vikuu tayari zimepewa mamlaka kisheria ya kusimamia ufadhili wa elimu ya juu nchini.
Katika muundo huo, wanafunzi hao wamewekwa katika makundi kwa kutegemea uwezo wao wa kulipa karo.
Wanafunzi pia wanatarajiwa kutuma maombi binafsi ya mikopo na ufadhili wa masomo na maombi yanazingatiwa kwa kutumia muundo wa kupima uwezo wao ili kubaini kiwango cha mahitaji ya kifedha ya mwanafunzi.
Hapo awali, wanafunzi waliofadhiliwa na serikali walikuwa wakilipa Sh16,000 kwa mwaka na kupata mkopo wa hadi Sh60,000 kila mwaka, chini ya Sheria ya Vyuo Vikuu.
Mashirika hayo yalisema wanafunzi kwa sasa wanapaswa kulipa Sh650,000 kwa mwaka bila ufadhili wa masomo wala basari.
“Zaidi ya hayo, vigezo vinavyotumika kumwezesha mwanafunzi kupata usaidizi wa serikali bado havijabainishwa. Kujua ni mwanafunzi gani aliye hatarini, masikinmi sana na asiye masikini sana ni changamoto,” yanasema katika kesi yao.
Mashirika hayo yalisema wanafunzi wapya wanakumbana na changamoto kuhusu ada za usajili, malazi, vifaa vya masomo na usalama wa matibabu wakati wa kuripoti kutokana na ukosefu wa miongozo inayotekelezeka.
Wanadai kuwa muundo huo ni kinyume cha katiba kwa vile unakiuka kanuni mbalimbali za katiba ikiwa ni pamoja na haki za msingi na uhuru, umekosa kuzingatia maslahi ya umma, na umeshindwa kukidhi matarajio halali ya wanafunzi kujiunga na vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu.
Wametaja Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor, Waziri wa Elimu Migos Ogamba, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu na KUCCPS kama washtakiwa katika kesi hiyo.