Wanaongoja kuchukua kazi ya Gachagua endapo atatimuliwa
MJADALA kuhusu anayeweza kuchukua nafasi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua, iwapo kuondolewa kwake madarakani kutafanikiwa, umeshika kasi, huku angalau mawaziri wawili wakiwa miongoni mwa wanaotajwa kuteuliwa kumrithi.
Takriban wabunge 291 wameunga mkono hoja ya Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse, ya kutaka Bw Gachagua aondolewe madarakani kama naibu rais, na hivyo kuzua mjadala kuhusu anayeweza kumrithi katika wadhifa huo.
Lakini huku zoezi la ushirikishaji wa umma kuhusu hoja hiyo likifanyika Ijumaa, majina ya Waziri wa Masuala ya Ndani Prof Kithure Kindiki, Mkuu wa mawaziri Musalia Mudavadi na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Anne Waiguru, yameibuka wakitajwa kama wanaoweza kuteuliwa naibu rais.
Wengine wanaopigiwa upatu kwa wadhifa huo ni pamoja na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro ambaye alikataa kuidhinisha hoja ya kuondolewa mamlakani kwa Bw Gachagua, Gavana wa Murang’a Irungu Kang’ata na mwenzake wa Embu Cicily Mbarire, Waziri wa Ardhi Alice Wahome, wote wanaotoka Kaunti ya Murang’a, kiongozi wa wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa ambaye ni mkosoaji mkali wa Bw Gachagua , mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga.
Viongozi wengi kutoka eneo la Mlima Kenya waliotia saini hoja ya kung’olewa madarakani kwa Gachagua wanataka kiongozi kutoka eneo hilo kuzingatiwa kwa wadhifa huo.
Takriban wabunge 48 kutoka eneo la Mlima Kenya walimtangaza Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki ambaye anatoka Mashariki ya Mlima Kenya kuwa msemaji wao, hata kabla ya kuwasilishwa kwa ilani ya hoja ya kutimuliwa kwa Gachagua.
‘Kwa kuzingatia hali iliyopo na dharura iliyo mbele yetu, kuna haja ya kuwa na uhusiano utakaojenga uhusiano kati yetu na Serikali ya Kitaifa kuhusu maendeleo,’ walisema wabunge hao katika taarifa yao iliyoashiria wanamchagua Prof Kindiki kama msemaji wao.
Lakini iwapo Dkt Ruto atamteua Prof Kindiki, itabidi azime mzozo unaotokota kati ya Mlima Kenya Mashariki na Magharibi, ambapo washirika wa Bw Gachagua wamemlaumu kwa kusababisha migawanyiko.
Naibu kiongozi wa chama cha DAP-Kenya Ayub Savula alisema kuwa kutokana hali ilivyo, ‘ Gachagua anaenda nyumbani.’
“Wabunge wengi wameamua kumtimua Bw Gachagua na sioni rais akifanya chochote kuwashawishi vinginevyo na sioni Riggy G akibadilika hata kama atanusurika.
“Uhusiano wake na viongozi umedorora. Wadhifa huu upatiwe Kindiki. Nafasi hiyo ni ya Mlima Kenya na anayefaa kuchukua nafasi hiyo ni Prof Kindiki. Yeye ni bora kuliko Gachagua. Amefaulu katika Wizara ya Masuala ya Ndani na anastahili kukwezwa,” Bw Savula aliambia Taifa Leo.
Alimkashifu Bw Gachagua kwa kudai kuwa “ kiongozi wa ‘Mrima’ (Mlima Kenya) ilhali anastahili kuwahudumia Wakenya wote.
Prof Kindiki anatoka Mlima Kenya Mashariki lakini imeibuka kuwa kuna msukumo kiongozi kutoka Magharibi kuchukua wadhifa huo kwa nia ya ‘kutuliza’ eneo hilo.
Magavana wa Kike chini ya vuguvugu la G7 wiki jana walimwidhinisha mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) anayeondoka Anne Waiguru kuteuliwa mgombea mwenza wa rais katika uchaguzi wa 2027, huku Taifa Leo ikifahamishwa kuhusu shinikizo zinazoendelea Gavana wa Kirinyaga achukue nafasi ya Bw Gachagua iwapo naibu rais atang’olewa. .
Wanaompigia debe Bi Waiguru wanaamini kuwa kama mwanamke, na mzaliwa wa Mlima Kenya Magharibi, Rais Ruto ‘anaweza kuua ndege wawili kwa jiwe moja,’ na kutuliza eneo hilo huku kukiwa na mvutano mkali kuhusu hoja ya kuondolewa madarakani kwa Bw Gachagua.
Vile vile, kuna mazungumzo ya kutaka Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi, ambaye ni wa tatu kwa hadhi serikalini, kuteuliwa naibu rais iwapo Bw Gachagua ataondolewa.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Richard Bosire aliambia Taifa Leo kwamba kuondolewa kwa Bw Gachagua afisini hakufanyi eneo la Mlima Kenya kunufaika moja kwa moja na wadhifa wa naibu rais, akiongeza kuwa rais ana uhuru wa kumteua Mkenya yeyote kushikilia wadhifa huo.
‘Ni jambo la kushangaza kusema wadhifa wa naibu rais ni hifadhi ya mlima. Hii itakuwa fursa nzuri ya kuwa na naibu rais kutoka eneo tofauti badala ya uongozi katika nchi hii kuonekana kuwa wa maeneo mawili,” alisema.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) David Sankok anasema kwamba huenda Rais Ruto akaamua kumteua Bi Wanga kama naibu wake lakini tu 2027 ikiwa ataimarisha ukuruba wake na kinara wa ODM Raila Odinga.