Habari za Kitaifa

Serikali ilivyotumia Sh1.6 trilioni kulipa madeni ndani ya mwaka mmoja

Na EDWIN MUTAI October 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI ilitumia Sh1.56 trilioni, pesa za mlipaushuru kulipia madeni ya umma katika mwaka wa kifedha uliokamilika Juni 2024, takwimu kutoka Hazina ya Kitaifa zilizowasilishwa bungeni zinaonyesha.

Kiasi hiki cha pesa kinawakilisha ongezeko la Sh363.9 bilioni kutoka Sh1.199 trilioni zilizotumika kulipia deni la umma katika mwaka uliopita wa kifedha wa 2022/2023.

Pesa zilizotumika kulipia madeni zimeongezeka baada ya serikali hii kuendeleza mtindo wa ukopaji madeni.

Serikali ya Kenya Kwanza imechukua mikopo 36 mipya, ya thamani ya Sh897.9 bilioni tangu iliposhika usukani Septemba 13, 2022.

Ripoti hiyo kuhusu madeni ya umma, ambayo hutolewa kila mwaka, inaeleza kuwa kudorora kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni pia kumechangia ongezeko la pesa zinazotumika na serikali kulipia madeni.

“Ongezeko hilo lilichangiwa na kupungua kwa thamani ya shilingi ya Kenya dhidi ya sarafu za kigeni haswa Dola ya Amerika katika miezi sita ya kwanza ya mwaka wa kifedha wa 2023/2024 na kulipwa kwa mkopo wa Eurobond wa Sh260 bilioni,” Waziri wa Fedha John Mbadi akasema katika ripoti hiyo.

Pesa ambazo serikali ilitumia kulipia madeni yaliyokopwa kutoka asasi za kifedha nchini ziliongezeka kwa kiwango cha asilimia 0.5.

Kwa ujumla, asilimia 68 za mapato ya kitaifa yalitumika kulipia madeni katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024 ikilinganishwa na asilimia 58.6 katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023.

Bw Mbadi alisema kuwa mzigo wa madeni unatarajiwa kuongezeka kutoka Sh10.582 trilioni katika mwaka wa wa kifedha wa 2023/2024 hadi Sh13.488 trilioni katika mwaka wa kifedha wa 2027/2028 “endapo serikali itaendelea kuchukua mikopo kugharamia shughuli zake.”

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa kiwango cha pesa ambazo Kenya ilikopa kutoka kwa taasisi za kimataifa za kifedha kilipanda katika mwaka wa kifedha wa 2023/2024 ikilinganishwa na mwaka wa kifedha wa 2022/2023.

“Pesa zilizotumika kulipa madeni yaliyokopwa kutoka mashirika ya kimataifa ya kifedha ziliongezeka kutoka Sh725.2 bilioni mnamo Juni 2023 hadi Sh100.9 bilioni mnamo Juni 2024,” ripoti hiyo inasema.