Makala

Kipyegon aliunda zaidi ya Sh30 milioni msimu mmoja 2024

Na GEOFFREY ANENE October 5th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

UKITAKA kujua talanta inalipa nchini Kenya, basi muulize Faith Kipyegon.

Kwa miezi mitatu tu, kati ya Julai na Septemba mwaka 2024, Kipyegon alivuna Sh33.2 milioni kabla ya ushuru kutolewa baada ya kushiriki riadha za Diamond League, Michezo ya Olimpiki na makala mapya ya mbio za wanawake pekee za Athlos NYC.

Fedha hizo hazijumuishi zawadi kutoka kwa serikali.

Kipyegon alianza msimu wake mwezi Juni wakati alishiriki mashindano ya kuingia Michezo ya Olimpiki na kunyakua tiketi katika mbio za mita 5,000 na 1,500m baada ya kushinda vitengo hivyo katika uga wa kitaifa wa Nyayo, Nairobi.

Kisha, Kipyegon akafungua msimu wa Diamond League kwa kishindo baada ya kuimarisha rekodi yake ya dunia katika 1,500m kutoka dakika 3:49.11 hadi 3:49.04 akitwaa taji la Paris nchini Ufaransa mnamo Julai 7.

Mshindi wa kila duru kwenye ligi ya Diamond League hutuzwa Sh1.2 milioni (Dola za Amerika 10,000).

Ukinakili rekodi ya dunia katika ligi hiyo jinsi alivyofanya Kipyegon, unaongezewa bonasi ya Sh6.4m (Dola za Amerika 50,000).

Kutoka Paris Diamond League, Kipyegon alirejea nyumbani na kuzamia maandalizi ya Olimpiki.

Mama huyo wa mtoto mmoja kisha alirejea mjini Paris kuwinda mataji ya 1,500m na 5,000m.

Kipyegon, ambaye alishinda mataji ya dunia ya 1,500m na 5,000m mwaka 2023 mjini Budapest nchini Hungary, aliridhika na medali ya fedha katika 5,000m kwenye Olimpiki mnamo Agosti 5 kabla ya kujizolea Sh6.4 milioni kwa kutawala 1,500m hapo Agosti 10.

Kisha, Kipyegon aliendelea na mawindo kwenye Diamond League, akinyakua taji la duru ya Golden Gala mjini Roma, Italia mnamo Agosti 30.

Mkimbiaji huyo, ambaye mume wake ni mshindi wa zamani wa nishani ya shaba ya mbio za mita 800 kwenye Olimpiki mwaka 2012 Timothy Kitum, alihifadhi taji lake la fainali ya Diamond League mjini Bruselles, Ubelgiji.

Mshindi wa fainali ya Diamond League hutia mfukoni Sh3.8m (Dola za Amerika 30,000).

Supastaa huyo kisha alifunga msimu kwa kuzoa Sh7.7 milioni (Dola za Amerika 60,000) kwenye shindano la mwaliko la siku moja la wanawake pekee la Athlos NYC ugani Icahn mjini New York, Amerika hapo Septemba 26.

Katika mbio za Athlos NYC zilizoanzishwa na kudhaminiwa na Alexis Ohanian, mume wa mwanatenisi Serena Williams, washindi walipewa pia kirauni ya fedha yenye thamani ya Sh3.2 milioni.

Kwa mujibu wa tovuti ya Runner’sWorld, washindi wote wa medali ya dhahabu kutoka Olimpiki 2024 walioshiriki Athlos NYC waliongezwa Sh7.7m.

Wakimbiaji wote 36 pia waliahidiwa kuwa watapokea asilimia 10 ya mapato kutoka makala hayo ya kwanza ya wanariadha wa kike.

Kabla ya Olimpiki 2024, Kipyegon, ambaye ni bingwa mara tatu wa dunia na Olimpiki mbio za 1,500m na dunia mbio za 5,000m, aliaminika kuwa na ukwasi wa Sh645m (Dola za Amerika 5 milioni) ambao bila shaka sasa umeongezeka.

Kipyegon amekuwa katika riadha ya watu wazima tangu mwaka 2014, ingawa nyota yake ilianza kung’aa akiwa katika riadha za chipukizi mwaka wa 2010.