Tafuteni kazi zingine, waambiwa wakazi baada ya mwanamke kufia kwenye mgodi wa dhahabu
WAKAZI wa Kambi Karaya, wadi ya Sekerr Pokot Magharibi wana majonzi baada ya mwanamke mmoja kufariki na wengine wawili kuponea baada ya kuzikwa wakiwa hai kwenye migodi ya dhahabu wakitafuta riziki Jumamosi.
Kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Pokot ya Kati (OCPD), Nelson Omwenga alisema kuwa wanawake watatu walikuwa wanachimba dhahabu kwenye migodi kabla ya kuanguka na kuua mmoja papo hapo.
“Wanawake wawili waliokolewa na wakazi wakiwa majeruhi,” alisema.
Bw Omwenga alisema kuwa mwili wa mwanamke huyo haujaondolewa kwenye migodi.
“Juhudi zinaendelea kuondoa mwili kutoka kwenye migodi,”alisema.
Diwani wa wadi ya Sekerr Jane Mengich aliwataka wakazi kutafuta mbinu mbadala za kujikimu.
“Tunaomba wakazi kujihusisha kwenye biashara zingine na wala sio kuchimba dhahabu,” alisema Bi Mengich.
Haya yanajiri huku visa vingi vya vifo kutokana na kusaka dhahabu vikiripotiwa Pokot Magharibi.
Wakazi hao hasa akina mama husukumwa kwenye migodi kutokana na hali ngumu ya maisha, umaskini na baa la njaa.
Ukosefu wa mvua na baa la njaa imesababishs akina mama, watoto na wakongwe kufanya kazi hiyo ya kubahatisha riziki kupitia kazi hiyo ngumu na hatari.
Shughuli hiyo pia imechangia wanawake wengi kuuawa na majangili wakiwa kwenye migodi.
Haya yanajiri baada ya akina mama wawili kuuawa na majangili wakisaka dhahabu katika kijiji cha Kases, eneo la Ombolion miezi miwili iliopita.
Julai mwaka huu, wanaume wawili walifariki kwenye migodi eneo la Kambi Karaya kwenye barabara kuu ya Lodwar –Kitale.
Mwaka wa 2022, akina mama 3 walifunikwa kwenye migodi katika eneo la Kambi Karaya kwenye barabara kuu ya Kitale -Lodwar.
Msichana mwenye umri wa miaka 15, Nakiru Ngolenyang alifunukiwa na migodi kwenye kijiji cha Narworwo, Lokesheni ya Alale, kaunti ndogo ya Pokot Kaskazini. Mwaka huo huo, wanawake 3 walifunikwa wakichimba dhahabu katika kijiji cha Nyelnyel eneo la Ptokou.
David Domungura mkazi wa Lami Nyeusi anasema kuwa mashimo ya dhahabu ni hatari.
Anasema kuwa akina mama wengi waliasi mashamba na kuanza kazi hiyo.
Kamishina wa Pokot Magharibi Khaliff Abdullahi anasema kuwa kumekuwa na ongezeko la vifo vinavyotokana na uchimbaji migodi na wiki hii serikali itapiga marufuku uchimbaji dhahabu haramu kwenye kaunti hiyo.
“Tumekuwa tukiwaeleza wakazi wasihusike kwenye uchimbaji dhahabu kinyume na sheria lakini hawasikii. Lazima tukomeshe tabia hii,” alisema Bw Khaliff.
‘‘Kila mtu anatamani kuwa tajiri lakini suala hili linachangia watoto wengi kuacha shule na wasichana kuolewa,’’ alilalamika.