Gachagua aamua kuanguka na Ruto, adai serikali imejaa ufisadi na mauaji ya kiholela
NAIBU Rais Rigathi Gachagua ameanzisha mashambulizi makali ya moja kwa moja dhidi ya Rais William Ruto, akisema serikali imejaa ufisadi na mauaji ya kiholela ambayo waliahidi kukomesha walipokuwa wakifanya kampeni.
Katika utetezi wake dhidi ya hoja kumtimua mamlakani, inayoonyesha kuwa uhusiano wake na Rais Ruto umeharibika kiasi cha kutorekebika, Bw Gachagua alisema hawezi kukubali ukatili dhidi ya raia.
Bw Gachagua alitaja mashtaka 11 dhidi yake kama ya kipuuzi na kuwataka wabunge wazingatie sakata za ufisadi ambazo alisema zimejaa serikalini.
Katika mkutano na wanahabari Jumatatu katika makazi yake rasmi ya Karen jijini Nairobi kabla ya kufika katika Bunge la Kitaifa kujitetea Jumanne, Bw Gachagua aliwashambulia Maspika wa Mabunge mawili – Moses Wetang’ula (Bunge la Kitaifa) na Amason Kingi (Seneti) ambao alilaumu kwa kuwa sehemu ya mpango wa umiliki wa hisa za serikali.
“Wananishtumu kwa kuzua mgawanyiko na mkabila ninapozungumza kuhusu hisa ilhali ninaendeleza tu yaliyomo katika mkataba wao wa kabla ya uchaguzi waliotia saini na Rais ambao ulikuwa umefichwa,” Bw Gachagua alidai.
Aliwashtumu Bw Wetang’ula na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi kwa kupatia kipaumbele masuala ya eneo lao la Magharibi, huku akimlaumu Bw Kingi kwa kujadiliana maslahi yake mwenyewe ili awe Spika wa Seneti badala ya kutetea maslahi ya eneo la Pwani anakotoka.
Pia, Bw Gachagua hakuwa na maneno mazuri kwa kinara wa upinzani Raila Odinga, ambaye alisema pia ameingia katika mpango wa hisa za serikali.
Alikuwa akirejelea kuundwa kwa Serikali Jumuishi ambayo viongozi wa zamani wa ODM waliteuliwa mawaziri.
Wanajumuisha waliokuwa naibu viongozi wa chama cha ODM Hassan Joho na Wycliffe Oparanya, aliyekuwa mwenyekiti wa kitaifa John Mbadi, aliyekuwa Mkurugenzi wa Masuala ya Kisiasa Opiyo Wandayi na aliyekuwa mwanachama wa bodi ya uchaguzi Beatrice Askul.
Naibu Rais anasisitiza kuwa hakukosea kushambulia hadharani Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) na maafisa wake wakuu inavyodaiwa katika mashtaka yaliyomo katika hoja ya kumtimua mamlakani akisema, alijifunza kutoka kwa bosi wake – Rais Ruto ambaye akiwa naibu rais alishambulia idara za usalama.
Mnamo Juni, Bw Gachagua alimkosoa Mkurugenzi Mkuu wa NIS Noordin Haji kuhusu maandamano ya kupinga serikali nchini, akiilaumu ofisi yake kwa kushindwa kutoa ushauri kwa kiongozi wa nchi ambao ungezuia ghasia na kuepusha vifo.
Hatua hiyo, ni sehemu ya mashtaka ya utovu wa nidhamu uliokithiri ambayo Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse ameorodhesha katika hoja yake kama msingi wa kuondolewa kwa Bw Gachagua.
“NIS ina jukumu muhimu sana katika kuhakikisha usalama wa nchi yetu. Ina jukumu la kukusanya taarifa za kijasusi na kuzitoa kwa vyombo vyetu vyote vya sheria ili kuhakikisha nchi inakuwa salama wakati wote.”
“Rais William Ruto wakati mmoja alipokuwa Naibu Rais alimkosoa Mkurugenzi wa Huduma ya Taifa ya Ujasusi wakati huo. Katika video nyingine, alimkosoa vikali Inspekta Jenerali wa polisi kwa utendakazi duni. Kwa hiyo nimejifunza kutoka kwa bosi wangu jinsi kazi hii inavyofanywa,” alisema.
Alisema kuwa yeye na rais wanakosolewa kila siku lakini hawalalamiki.