Afya na Jamii

Ole wako kama soda haikupiti, wataalamu wameonya ina madhara ya kiafya

Na WANGU KANURI October 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WATAALAMU wameonya kuhusu uraibu wa unywaji soda kila wakati wakisema kinywaji hicho kinaweza kusababisha madhara ya kiafya.

Joy Ouma, mtaalamu wa lishe katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan anasema kuwa vinywaji kama hivi huongeza nguvu mwilini kupita kiasi na kuathiri hisia ya mhusika.

Anaeleza, “Kiwango cha sukari katika soda huongeza sukari mwilini haraka na hivyo kuyumbisha hisia.

“Vilevile, waraibu wa vinywaji hivyo hujipata katika hatari ya kupatwa na shida ya unene kupita kiasi, ugonjwa wa kisukari, maradhi ya moyo, kuathiriwa kwa figo, magonjwa yanayoathiri meno.”

Dkt Ouma anaongeza kuwa waraibu wanaweza kuathirika shida ya kupoteza maji mwili, ongezeko la asidi na gesi tumboni.Je, vinjwaji kama soda vina manufaa yoyote mwilini?

Mataalamu huyo anajibu hivi: “Vinywaji hivi havina kalori yoyote. Havina madini yenye manufaa kwa mwili wa mwanadamu.”

Vilevile, Dkt Ouma anasema vinjwaji kama soda vinasheheni kemikali kama vile sacralose aspartame na saccharin husababisha mwasho mwilini.

“Hii ni hatari kwa afya ya mwanadamu,” anasema. Je, kuna tabaka la watu ambao huathirika zaidi na madhara ya unywaji soda? Dkt Ouma anajibu kuwa watoto, vijana waliobaleghe, wazee na wanawake wajawazito ndio ambao huathirika zaidi.

“Kwa wanawake wajawazito, unywaji soda kupita kiasi unaweza kusababisha aina fulani ya ugonjwa wa kisukari ambao unaweza kuathiri akina mama hao na watoto wao wakiwa tumboni,” akasema.

Na wazee wanaokunywa soda kila mara huathiriwa na maradhi ya mifupa na yale ya moyo. Kwa hivyo, Dkt Ouma anashauri kwamba wala wanaotaka kupunguza kiwango cha soda wanaokunywa wanaweza kunywa sharubati na hata maziwa chachu au yale yasiyo chachu.

“Aidha, wanaweza kuanza kuzoea kunywa maji, supu au chai ya kiasili. Kwa kufanya hivyo, waraibu wanaweza kupunguza hamu ya kutaka kunywa soda,” anaeleza.

Vile vile, Dkt Ouma anashauri, waraibu wa soda wanaweza kupunguza mazoea ya kuhudhuria hafla za kijamii ambako vinywaji kama hivyo hutumiwa.

Mtaalamu huyo pia anashauri kuwa waraibu wa soda wanaweza kuelimishwa au kuhamasishwa kuhusu madhara ya vinywaji kama hivyo kwa afya.

“Kupitia mafunzo na uhamasisho kama huo, hatimaye watu kama hawa wanaweza kukinai soda na kujiepusha kabisa na madhara yake,” Dkt Ouma anaeleza.