Wasiwasi mbu waenezao malaria wakipata kinga sugu na kukosa kusikia dawa
WANASAYANSI wamegundua kwamba aina ya mbu anayelaumiwa kwa maambukizi ya malaria Mashariki na Kusini mwa Afrika ameendelea kupata kinga sugu dhidi ya dawa iliyotumika kwa muda mrefu katika maeneo haya.
Anopheles funestus ni mojawapo ya aina za mbu wanaoeneza malaria Mashariki na Kusini mwa Afrika ikiwa ni pamoja na Kenya na wanasayansi wanaonya kuwa kugunduliwa huku kunaibua wasiwasi kuhusu ufanisi wa dawa za kuua wadudu katika vita vya kudhibiti malaria.
Watafiti waligundua kwamba mdudu huyo anabadilika kijeni ili kukuza kinga kwa dawa iliyopigwa marufuku lakini inaendelea kuathiri mazingira.
Utafiti uliongozwa na Chuo Kikuu cha Glasgow na Taasisi ya Afya ya Ifakara nchini Tanzania. Ni mara ya kwanza kwa mabadiliko hayo kurekodiwa katika aina hii ya ya mbu ambayo inahusishwa na maambukizi ya malaria Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Mabadiliko yaligunguliwa watafiti walipokuwa wakifuatilia mbu nchini Tanzania ili kuelewa vyema tofauti za kijeni katika aina za mbu.Mabadiliko mapya sugu katika aina hii ya mbu yanahusishwa na uchafuzi wa mazingira na historia ya dawa maarufu iliyofahamika kama DDT.
DDT ilitengenezwa kama dawa ya kwanza ya kuua wadudu katika miaka ya 1940. Hapo awali ilitumiwa kwa ufanisi mkubwa kupambana na malaria na magonjwa mengine ya binadamu yanayoenezwa na wadudu miongoni mwa wanajeshi na raia.
Dawa hiyo ilipigwa marufuku na serikali ya Kenya, kwanza mwaka wa 1976 kwa matumizi ya mifugo na baadaye mwaka wa 1986 kama dawa ya kilimo.
“Utafiti wetu unaibua wasiwasi kuhusu ufanisi wa mbinu za sasa za kudhibiti malaria, ambazo zinategemea sana dawa za kuua wadudu. Kuelewa maendeleo ya dawa za kuua wadudu ni muhimu katika kupambana na malaria, ugonjwa ambao unaua mamia ya maelfu ya watu kila mwaka, hasa katika Afrika,” alisema Joel Odero, kiongozi wa na mwanafunzi wa uzamifu katika Chuo Kikuu cha Glasgow.
Odero pia ni mtafiti katika Taasisi ya Afya ya Ifakara.
“Utafiti unaonyesha jinsi hali ya mazingira kama vile uchafuzi kutokana na DDT unaweza kuzua changamoto za afya ya umma. Kuibuka kwa mbinu mpya za kinga kunaweza kutishia miongo kadhaa ya maendeleo yaliyopatikana katika kupunguza maambukizi na vifo vya malaria,” aliongeza.
Odero alisema kuwa mbu aina ya Anopheles funestus hivi majuzi alilaumiwa kwa kuongezeka kwa maambukizi ya malaria katika nchi kama Kenya.
Fredros Okumu, mtaalamu wa wadudu, ambaye anafanya kazi kama mkurugenzi wa sayansi katika Taasisi ya Afya ya Ifakara, aliiambia Taifa Leo kwamba utafiti wa ufuatiliaji unahitajika.
“Utafiti wa ufuatiliaji wa haraka unahitajika kufuatilia mageuzi ya kinga ya DDT na kuamua kama aina hii inaweza kutokea katika familia nyingine za dawa za kuua wadudu ambazo kwa sasa zinasambazwa katika bara la Afrika,” alisema Okumu.