Gachagua alivyocheza kanda za video za Ruto kujaribu kujiokoa
NAIBU Rais Rigathi Gachagua Jumanne jioni aliwasilisha utetezi wake wa mwisho kwa Bunge ambapo washirika wa Rais Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga waliungana kumkomoa.
Gachagua alilazimika kuomba radhi wabunge waliomkemea kwa kufanya kikao na wanahabari Jumatatu kuzungumzia kesi yake, wakimlaumu kwa kudunisha mamlaka ya Bunge.
Naibu Rais katika nyakati kadhaa aliamua kucheza kanda za video ambazo zilionekana kumwingiza Rais Ruto kwenye zogo hilo, katika juhudi za kujinasua kutoka kwa kinywa cha mamba.
Hata hivyo, huku akicheza video hizo, aliepuka zile ambazo zingemchongea hata zaidi kwa Wabunge.
Miongoni mwa video alizocheza zilijumuisha ya rais akiita mawaziri na makatibu wa wizara kuwa wavivu baada ya kuwafungia nje katika mikutano miwili wakati wa vikao Nanyuki na Ikulu ya Nairobi.
Pia alicheza video ikimuonyesha Rais Ruto akimshambulia wazi wazi Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi (DCI) George Kinoti, ambaye alilazimika baadaye kujiuzulu na akakumbusha wabunge kwamba ilikuwa si haki kwa jinsi alivyomuingia afisa huyo.
“Mimi nilijifunza kutoka kwa bosi wangu, rais, ambaye alinifunza kukemea utendakazi duni wa maafisa wa umma. Lakini hamumtimui kwa makosa hayo, ila mimi,” akaambia Bunge.
Huku akijitetea dhidi ya madai ya kudhalilisha Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ujasusi Noordin Haji, Bw Gachagua alishikilia kwamba Bw Haji alifeli kwa kukosa kumshauri Rais kuhusu hisia za wananchi kuhusu mswada tata wa Fedha, ambao uliishia katika maafa na mali kuharibiwa.
“Hata leo, ninashikilia kwamba mkuu wa ujasusi alifaa kujua kabla ya maandamano kwamba umma ulikuwa unapinga kabisa Mswada wa Fedha na alistahili kumjuza Rais kuhusu hilo,” akaambia wabunge.
Kwenye madai kwamba amejilimbikizia mali ya Sh5.2 bilioni katika muda wa miaka miwili ambayo amekuwa afisini, alisema kwamba nyingi ya mali anayodaiwa kumiliki ni kakake marehemu Nderitu Gachagua kama ilivyonakiliwa kwenye wosia wa urithi.
Aligusia madai kwamba anamiliki hoteli ya Olive Garden akisema kwamba ni uongo.
“Hiyo hoteli ilikuwa ya kakangu na kwa hivyo haijawahi kuwa mali yangu,” akasema na kuendelea, “pindi alipoaga dunia, kakangu aliacha wosia ambapo alinichagua kama msimamizi wa familia yake hivyo akaniteua kuwa mmoja wa wasimamizi wa mali zake.”