Maoni

MAONI: Ruto asinyamaze, aeleze Wakenya ‘dhambi’ zilizomkosanisha na naibu wake

Na LEONARD ONYANGO October 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

DHAMBI ambazo Naibu wa Rais Rigathi Gachagua anadaiwa kutenda na kusababisha wabunge kumng’oa afisini, hazina mashiko.

Mambo anayodaiwa kufanya, yamekuwa yakifanywa na wanasiasa kwa miaka na mikaka bila kuchukuliwa hatua.

Viongozi kupewa kandarasi na serikali, kufuja fedha za umma, kuchukua hongo kutoka kwa mabwanyenye wanaosaka zabuni serikalini na kutoa nafasi za kazi kwa misingi ya kikabila ni miongoni mwa maovu ambayo yamekuwa ya kawaida humu nchini bila wahusika kuchukuliwa hatua.

Inakadiriwa kuwa zaidi ya Sh140 billion – ambazo ni sawa na asilimia 36 ya jumla ya mgawo ambao hutolewa kwa serikali za kaunti – zinaibiwa kila mwaka na maafisa serikalini.

Kwa mfano, ripoti ya hivi karibuni ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) inaonyesha kuwa kiasi cha fedha zinazotolewa kama hongo ili kupata kazi serikalini kimeongezeka maradufu ndani ya kipindi ambacho serikali ya Kenya Kwanza imekuwa mamlakani.

Kwa sasa Mkenya ni sharti atoe hongo ya kiasi kisichopungua Sh163,000 ili kupata ajira serikalini. Wakenya wanaotafuta baadhi ya huduma za serikali wanalazimika kulipa hongo ya hadi Sh70,000.

Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Matumizi ya Fedha za Umma amekuwa akitoa ripoti tele zinaoonyesha jinsi ufisadi unatokota katika Serikali ya Kitaifa na Kaunti.

Ufisadi umekolea kiasi kwamba mwaka jana Mkaguzi Mkuu wa Matumizi ya Fedha za Umma Nancy Gathungu alilazimika kuwasihi wezi wa fedha za umma wanaoponyoka mkono wa sheria kuwekeza humu nchini ili kuwapa Wakenya nafasi za ajira.

Hiyo ni baadhi tu ya mifano ya kuonyesha jinsi ufisadi umekolea na kutapakaa kila kona.

Hivyo, hatua ya wandani wa Rais Ruto kudai kwamba waliamua kumng’oa Bw Gachagua kwa sababu alifanya biashara na serikali ni kufumba macho Wakenya.

Madai kuwa kauli ya Bw Gachagua kwamba ‘serikali ni sawa na kampuni ambapo ni wenyehisa tu wanafaidi’ hayana uzito wa kusababisha kumtimua afisini kwa kisingizio kwamba anagawanya Wakenya.

Tumeona hata wandani wa Rais Ruto wakitusi baadhi ya jamii kwa misingi ya tohara bila kuchukuliwa hatua.

Ukichunguza kwa makini, utabaini kuwa baadhi ya ushahidi uliotolewa Bungeni dhidi ya Bw Gachagua ni video za hotuba alizotoa hata baada ya vigogo wa Kenya Kwanza kuanza mchakato wa kumtimua.

Uhasama baina ya Bw Gachagua na wandani wa Rais Ruto ulianza hata kabla ya kuwasilishwa bungeni Mswada wa Fedha wa 2024 uliotupiliwa mbali kufuatia maandamano yaliyoongozwa na vijana barobaro, almaarufu Gen Z.

Hiyo inaashiria kwamba kiini cha uhasama baina ya Bw Gachagua na Dkt Ruto ni tofauti na mambo yaliyowasilishwa bungeni dhidi ya Naibu wa Rais.

Hivyo, Wakenya wana haki ya kuelewa kilichosababisha Dkt Ruto kumtema Bw Gachagua.