Jamvi La Siasa

Ngome ya Ruto yakosoa kutimuliwa kwa Gachagua: ‘Fomu zilikuwa tayari zimesainiwa’

Na WAANDISHI WETU October 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

BAADHI ya Wakazi wa kaunti za Kaskazini mwa Bonde la Ufa ambazo ni ngome ya kisiasa ya Rais William Ruto wamesikitishwa na kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na wamelilaumu Bunge la Kitaifa kwa hatua hiyo ya Jumanne usiku.

Huku baadhi ya watu wakiunga mkono uamuzi wa kuondolewa mamlakani kwa Bw Gachagua, wengine walionyesha kutoridhika, wakishutumu Bunge kwa kutawaliwa na siasa.

Katika Kaunti ya Turkana, wakazi wa Mji wa Lodwar sasa wanataka Bunge la Kitaifa liwasilishe hoja ya kumuondoa Rais William Ruto pia, wakisema utawala wa United Democratic Alliance (UDA) umefeli Wakenya.

Katika Kaunti ya Baringo, wakazi walionyesha kutoridhishwa na kuondolewa kwa Bw Gachagua wakisema wabunge hawakuwa na ushahidi wa kutosha wa kumtimua.

Bw Cheseru Kipsimta alikashifu Bunge, akisema lilifeli katika jukumu lake la kutunga sheria, na kukubali kudanganywa na Rais Ruto ili kutatua masuala ya kisiasa.

“Mashtaka zaidi ya 11  dhidi ya DP  hayakuwa na msingi. Tunahofia kuwa wabunge hao walikuwa wakifanya kazi kwa kulazimishwa na mtu fulani,’ akasema Bw Cheseru.

Yassin Hamisi kutoka Mji wa Kabarnet alisema jambo zuri ambalo Rais alipaswa kufanya ni kusameheana na naibu wake iwapo alimdhulumu ili kudumisha amani na maendeleo ya nchi badala ya kumuondoa ofisini.

Katika Kaunti ya Pokot Magharibi, wakazi ambao hawakuidhinisha uamuzi wa Bunge la Kitaifa kuhusu kuondolewa kwa Bw Gachagua walisema Jumatano kwamba bado wana matumaini katika Seneti.

“Mashtaka yalikuwa na nia mbaya.Wabunge wote walikuwa Bungeni, tofauti na siku nyingine yanapojadiliwa mambo muhimu yanayohusu nchi. Bunge lilikuwa limejaa na ilionekana kama siku ya kiyama. Wengine hawakuzungumza hata neno moja kutoka 8 mbili asubuhi hadi saa tatu usiku. Hatukuwachagua kwenda kutimua watu bila idhini yetu,” akalalamika Ashiono Wendo, mkazi wa Kapenguria.

Alitaja ushiriki wa umma ambao ulifanywa Ijumaa na Jumamosi wiki jana kama batili kwa kuwa ulivyofanywa kabla ya Bw Gachagua kujitetea.

“Fomu zilikuwa tayari zimesainiwa. Hatukusikia upande wa Rigathi wakati wa ushiriki wa umma. Tunahitaji Adani na mambo ya elimu ya juu yashughulikiwe. Ni watu wachache tu walishiriki katika ushiriki wa umma ilhali  ni Wakenya tuko wengi,” akasema.

Mkazi mwingine Nickson Kaboro alisema Bunge lilikuwa  dharau kubwa kwa Wakenya.

“Wabunge hawakufuata utaratibu kwa sababu hatuoni makosa ya Rigathi. Alimsaidia Rais Ruto na sasa amefutwa kazi,” alisema.

Rosaline Ashiroi kutoka Kapenguria, hata hivyo, aliunga mkono kuondolewa kwa naibu rais akisema amekuwa akimkosea heshima bosi wake.

Katika Kaunti jirani ya Turkana, wakazi wa Mji wa Lodwar sasa wanataka Bunge la Kitaifa kuwasilisha hoja kuhusu kutimuliwa kwa Rais William Ruto wakisema kuwa utawala wa UDA umefeli Wakenya.

Bw Joseph Egelan alisema kuwa kumuondoa naibu rais pekee hakuwezi kutatua matatizo ya Wakenya wa kawaida.

Bw Egelan alisema kwamba sababu nyingi ambazo Bunge la Kitaifa lilitegemea kumtimua Bw Gachagua zinahusu Rais na Wabunge.

Alisema uongozi wa UDA haujajifunza kutokana na maandamano makubwa ya mwezi Juni ya kupinga Mswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2024 ambapo watu walipoteza maisha, wengine kutekwa na haki bado haijapatikana.

Bi Jane Longor alitoa wito kwa wabunge kutanguliza matatizo yanayowakabili Wakenya badala ya tofauti za  Naibu Rais na Rais.

Katika Kaunti ya Trans Nzoia, baadhi ya wakazi hawakuunga mkono mchakato wa kuondolewa kwa Bw Gachagua wakisema ulifanywa haraka na ulikuwa wa  kisiasa.

“Kulikuwa na haraka gani ya kumuondoa hata bila kushirikisha wananchi ipasavyo? Hii inaonyesha kuwa hawakujali maoni ya Wakenya,” alisema Kennedy Soita.

Ripoti ya Sammy Lutta, Oscar Kakai na Evans Jaola

Tafsiri: Benson Matheka