Hofu ya kufungwa shule mapema kutokana na uhaba wa pesa
SHULE za Upili huenda zilazimike kufunga mapema baada ya serikali kukosa kuachilia pesa zinazohitajika kuendeleza shughuli kwa muhula wa tatu.
Shirikisho la Wakuu wa Shule za Upili (KESSHA) limetoa tahadhari, likisema kwamba shule zinashindwa kununua bidhaa za kimsingi kwa maandalizi ya mtihani ujao wa KCSE na mitihani ya kufunga mwaka kwa watahiniwa.
Kati ya Sh22,244 kwa mwanafunzi zilizokuwa zinatarajiwa chini ya mpango wa ufadhili wa elimu, serikali ilituma Sh15,192 pekee ambapo hapo pia waliagiza Sh3,850 zielekezwe kwenye ujenzi wa muundomsingi. Hii inaacha Sh11,342 pekee za kutumiwa kwa shughuli za kila siku.
Hii ni licha ya ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaojiunga na shule za upili kila mwaka, huku ugavi wa pesa nao ukipungua serikali ikishikilia kwamba inatatizika kupata pesa za kulipa kwa mkupuo mmoja.
“Tayari kuna matatizo makubwa ya kifedha shuleni na haiwezekani kukamilisha muhula ikiwa pesa zilizobakia hazitatolewa upesi. Inasikitisha kwamba wafanyakazi wa shule watakosa mishahara. Tuna wasiwasi kwamba mzogo wa madeni shuleni unaendelea kuwa mzito kiasi cha kutobebeka,” akaonya Willy Kuria, mwenyekiti wa Kessha.
Uchunguzi wa Taifa Leo umebaini kwamba tayari baadhi ya shule zimeshapanga kuachilia wanafunzi Oktoba 18, 2024 ili kuepuka kukosa mahitaji ya kukidhi wanafunzi.