Makala

Wasichana waliopata mimba wakiwa wadogo waungana ili kusaidiana

Na KNA, LABAAN SHABAAN October 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

KAUNTI ya Narok (asilimia 28) ni moja ya kaunti nne nchini zenye visa vingi vya mimba za utotoni baada ya Samburu (asilimia 50), Pokot Magharibi (asilimia 36) na Marsabit (asilimia 29); kulingana na ripoti ya hali ya afya 2022 iliyofanywa na shirika la Kenya Demographic Health Survey (KDHS).

KDHS ni shirika la kukusanya takwimu kuhusu jamii na afya ili kusaidia kubuni sera na kutathmini mipango ya serikali.

Wadau husika wanahisi kuna mabadiliko mazuri kuhusiana na mikakati ya kudhibiti mimba za udogoni Narok

Gatuzi hili liliongoza kwa mimba za mapema mwaka wa 2014 kwa asilimia 40.

Takwimu katika Idara ya Afya zinaonyesha kuwa zaidi ya wasichana 4,000 huenda hospitalini kwa huduma za kliniki ya ujauzito katika zahanati mbalimbali Kaunti ya Narok kila mwaka.

Wanaishi vipi

Yamkini mtu anaweza kujiuliza kina mama hawa wachanga huenda wapi baada ya kutungwa mimba kabla ya kuwa watu wazima.

Kundi moja la wasichana wachanga limeamua kushirikiana kuboresha maisha yao baada ya kujifungua; linaitwa Binti Shupavu na lina makao yake eneo la Sekenani, Kaunti ndogo ya Narok Magharibi.

Shirika hili lenye makumi ya wanachama limewezesha wasichana hawa kutengeneza bidhaa mbalimbali ili kujichumia riziki.

Miongoni mwa bidhaa wanazounda ni sabuni ya maji, mapambo, sodo na nepi.

Mmoja wa wasichana hao, Diana Kiminta, mwenye umri wa miaka 19 anafunguka kuwa alipata mimba akiwa kidato cha pili na alilazimika kuacha shule ili kumlea mtoto.

Alirudi shuleni

Baada ya chifu kuingilia kati, wazazi wake walilazimika kumrudisha shuleni na akafaulu kufanya mtihani wa kitaifa 2023.

Nusura aozwe na nyanya yake ambaye walikuwa wanaishi pamoja. Mlezi huyu alikuwa akilemewa kumudu mahitaji ya maisha yao kila siku.

Kwa bahati nzuri, rafiki yake akamtambulisha kwa kundi la Binti Shupavu ambapo aliungana na wasichana wengine wachanga kujihusisha na biashara.

“Tangu nijiunge na kundi hili Februari 2024, nimejifunza mambo mengi sana yanayoweza kunisaidia kujisimamia. Kundi hili limefufua matumaini yangu ya kuwa mwanabiashara mkubwa siku zijazo,” alisema.

Tukio sawa lilimkuta Mercy Keleto, 21, ambaye alipata ujauzito alipojiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN).

“Nilikuwa na umri wa miaka 19 nilipopata ujauzito. Wazazi wangu walikuwa na matumaini makubwa lakini yakasambaratika baada ya kupata mimba. Waliacha kunisaidia kuendelea na chuo ikabidi niache masomo,” alikiri.

Keleto anasema alijiunga na kundi hili mapema mwaka wa 2024. Alipokewa vizuri na kuelekezwa chini ya mpango wa ushauri nasaha.

Binti mwingine aliyetungwa mimba akiwa mdogo ni Susan Wanjiru. Baadaye aliishia kuacha shule kabla ya kufanya mtihani wa mwisho.

Yeye ni mmoja wa viongozi wa kundi. Anasema waliungana ili kupeana moyo baada ya ndoto zao kukatizwa wakiwa wadogo.

“Hatua ya kuungana imetusaidia kujiamini. Tunaambiana kuhusu ndoto zetu huku tukipatiana motisha ya kuwa maisha mema ya usoni. Ndiyo sababu tulishikana mkono,” alisema.

Wanapigwa jeki

Mabinti hawa shupavu wamefaidika na misaada kutoka kwa mashirika na watu mbalimbali baada ya kuanza shirika lao.

Wanjiru anatambua msaada ambao wanapokea kutoka kwa shirika la kijamii la Population Services Kenya.

Ni shirika ambalo huangazia masuala ya uzazi na afya hasaa kuhusu wasichana wadogo walio katika hatari ya kuathiriwa.

Wamepokea msaada wa kuanzisha biashara, kupata karo, elimu na ushauri nasaha.

Vile vile, Wanjiru anawaomba wasichana wasijihusishe na mahusiano ya kimapenzi wakiwa shuleni sababu hii itasitisha safari yao ya elimu wakiwa wachanga.