Habari za Kitaifa

Kesi tano za kupinga kutimuliwa kwa Gachagua zatua kwa Jaji Mkuu Koome

Na RICHARD MUNGUTI October 11th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KESI tano za kupinga kutimuliwa kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua zimepelekwa kwa Jaji Mkuu Martha Koome, ili ateuea  majaji wa kuzisikiliza.

Jaji wa Mahakama Kuu Lawrence Mugambi alikubaliana na Bw Gachagua na walalamishi wengine kwamba masuala yaliyoibuliwa katika kesi hizi ni mazito na yanafaa kuamuliwa na jopo la majaji watatu.

“Ni maoni yangu kwamba masuala yaliyoibuliwa ni mazito ya kikatiba, kwa hivyo ninashawishikwa kuyapeleka kwa Jaji Mkuu ili kuunda jopo la majaji kuyasikiliza,” Jaji alisema.

Kulingana na jaji huyo, suala la ushiriki wa umma, ambalo Bw Gachagua ameshikilia kuwa haukotosha, ni suala zito ambalo linafaa kusikilizwa na majaji watatu.

Jaji Mugambi alisema kutimuliwa kwa Naibu Rais ni suala la maslahi ya umma na kuongeza kuwa linaibua changamoto za kipekee ikiwa ni pamoja na muda wa kulishughulikia, ushiriki wa kutosha wa umma na iwapo Bunge lilikuwa limeundwa ipasavyo.

Naibu Rais, kupitia  Wakili Mkuu Paul Muite, alikuwa ameomba mahakama  kutoa uamuzi kuhusu suala la ushirikishaji wa umma ulioendeshwa na Bunge kabla ya kura ya kumtimua Bw Gachagua, akiteta kuwa halikutimiza kiwango kinachohitajika.

Mbali na ushiriki wa umma, Bw Muite amepinga kanuni ya Bunge la Kitaifa, ambayo inaruhusu siku kumi na mbili pekee kwa suala hilo kushughulikiwa na kuwasilishwa kwa Seneti.

Kulingana na Bw Muite, Naibu Rais hakupewa muda wa kutosha kujibu masuala hayo, ambayo yaliwekwa kwa umma kuunda msingi wa kuondolewa kwake ofisini na kwa maoni yake, alifaa kupewa angalau siku 12 kujiandaa kwa utetezi wake.

Alisema suala la ushirikishaji wa wananchi ni suala lililopita na mahakama haina mamlaka ya kuamua jambo hilo katika hatua hii.