Anavyopambana na mabroka wa vitunguu
EUNICE Mutai ni mmoja wa wakulima waliojitolea katika kilimo cha vitinguu aina ya spring onions kijijini Lekimbo, kaunti ndogo ya Bomet Mashariki.
“Awali niliona wakulima wengine wanafanya vizuri ikabidi nijaribu,” alifunguka mkulima aliyeanza mwaka wa 2018.
Katika shamba lake la nusu ekari, Bi Mutai anakuza mimea hii katika viwango tofauti kuhakikisha anavuna baada ya kila wiki mbili.
“Hiyo ndiyo siri yangu ya kuongeza faida,” anaarifu.
Udongo wenye rutuba eneo hili humwepusha na gharama ghali ya mbolea. “Almuradi ninapalilia vizuri, mimea yangu hunawiri,” anaeleza kwa ujasiri.
Hali nzuri ya anga eneo hili humwezesha kuvuna baada ya kila miezi miwili pindi apandapo.
Changamoto kubwa anayopitia ni vimelea na mgonjwa ambayo husumbua mmea huu.
“Mimi huhakikisha udongo hauna unyevu mwingi ili kuepuka maradhi hatari,” anasema.
Changamoto ya bei
Hata katika kipindi ambacho bei ya vitunguu viko juu, Bi Mutai na wakulima wenzake wanapitia changamoto hasaa kutoka kwa mabroka.
“Nyakati nyingine bei huwa chini sana. Hapo matatizo kwetu huwa mengi,” anadokeza.
Kwa kawaida yeye huvuna magunia 15 ya vitunguu kila msimu. Bei zinapopanda kufika Ksh 15,000 kwa kila mfuko wa kilo 200, mapato yake huwa makubwa.
Hata hivyo, bei zinaweza kushuka hadi kufikia Ksh 7,000, huku madalali wakivuna pakubwa.
“Lakini mara kwa mara madalali wanataka kununua mazao yetu kwa bei ya chini ya Ksh 5,000, na hii inatuumiza sana,” Bi Mutai analalamika.
Madalali hawa mara nyingi huuza mazao jijini Nairobi, ambapo mahitaji ni makubwa.
Licha ya kupokea usaidizi wa mbinu bora za ukulima kutoka kwa maafisa wa ugani wa kaunti, wakulima kama Bi Mutai wanaitaka serikali ya kaunti kuweka udhabiti wa bei.
“Tunataka kuuza kwa angalau Ksh 7,000 ili kuepuka hasara,” anasisitiza.
Mmoja wa mabroka ni Bi Sharon Ruto ambaye amekuwa katika biashara hii tangu 2017.
“Mimi hutembelea wakulima katika Bomet ili kuwaambia kuhusu muunganisho wangu na soko,” Bi Ruto anaeleza.
Wakati mwingine Bi Ruto huwalipa wakulima mapema ili kuwa na uhakika wa kunasa soko hili – ni njia yake ya kukabili washindani.
“Soko linapendelea vitunguu vya ukubwa wa wastani, si vidogo sana au vikubwa sana,” anabainisha.
Kukabili Changamoto
Wakulima hawa hawahifadhi mavuno yao: wanunuzi huzikusanya moja kwa moja kutoka mashambani.
Mtaalamu wa Kilimo Bomet Mashariki, Bw Joel Kibet anawataka wakulima kuunda vyama vya ushirika ili kupata uwezo thabiti wa kupata bei bora sokoni.
“Hii itawasaidia kupata bei ya juu na kuwadhibiti madalali wanaokiuka kanuni za viwango na bei,” anaeleza.
Madalali mara nyingi hurefusha mifuko ili kuongeza faida zao, wakiwapunja wakulima desturi hii ikikithiri.