Yadaiwa Gachagua kunusurika huko Seneti ni miujiza
BAADA ya Naibu Rais Rigathi Gachagua kufeli kuzima kuwasilishwa kwa hoja ya kumtimua afisini katika Seneti, sasa hatima yake iko mikononi mwa maseneta 67 wa bunge hilo.
Akikatalia mbali ombi la jopo la mawakili wa Bw Gachagua, wakiongozwa na Paul Muite, Jaji wa Mahakama Kuu Lawrence Mugambi aliagiza kuwasilishwa kwa kesi zote 22 zinazopinga kung’atuliwa kwa kiongozi huyo kwa Jaji Mkuu Martha Koome ili abuni jopo la majaji watatu kuzisikiza na kuziamua.
Alisema kesi hizo zinaibua masuala mazito ya kikatiba na yanayosheheni masilahi ya umma na hivyo yanayopasa kuamuliwa na zaidi ya Jaji mmoja.
Jaji Mugambi alitoa uamuzi huo Ijumaa siku tatu baada ya Bunge la Kitaifa kupitisha hoja ya kumtimua Bw Gachagua na siku moja baada ya Spika wa Seneti Amason Kingi kuagiza kuwa hoja hiyo itashughulikiwa na maseneta mnamo Oktoba 16 na Oktoba 17; siku za Jumatano na Alhamisi.
Kwenye taarifa, Bw Kingi pia alipiga marufuku safari zozote za maseneta na wafanyakazi wa asasi hiyo nje ya nchi kuhakikisha kuwa maseneta wote wanashiriki katika mijadala na upigaji kura kuamua hatima ya hoja hiyo.
Aidha, alizima kufanyika kwa vikao vyovyote vya Seneti nje ya Nairobi kati ya Oktoba 8 hadi 19 mwaka huu.
“Mjuavyo, Seneti itahitaji kufanya maamuzi kuhusu shughuli muhimu siku zijazo. Kulingana na uzito wa suala hili, ni muhimu kwa maseneta wote kuwepo na kushiriki,” akasema katika taarifa hiyo.
“Kwa hivyo safari za maseneta na maafisa wa seneti nje ya nchi zimesitishwa,” Bw Kingi akaongeza.
Kulingana na kipengele cha 150 (2) kuhusu hitaji la kuondolewa afisini kwa Naibu Rais, hoja ya kufikinisha hatua hiyo inapasa kuungwa mkono na angalau thuluthi mbili ya maseneta wote 67 wakiwemo maseneta maalum.
Isitoshe, tofauti na hoja za kuwaondoa afisini magavana ambazo hupigiwa kura na maseneti 47 wanaowakilisha kaunti pekee, hoja kama hii itapigiwa kura na maseneta wote 67, wanaojumuisha maseneta maalum.
Kwa hivyo, mnamo siku ya Alhamisi hoja hiyo inahitaji kuungwa mkono na angalau maseneta 45 ndiposa ipite na ili Bw Gachagua akome kushikilia wadhifa wa Naibu Rais.
Kwa upande mwingine, ili hoja hiyo ianguke Bw Gachagua atahitaji kuungwa mkono na angalau maseneta 23 ndiposa hitaji la kikatiba la thuluthi mbili ya maseneta likose kutimizwa.
Wadadisi wanasema, kwa kuzingatia jinsi wabunge walipigia kura hoja hiyo Oktoba 8, itakuwa kibarua kigumu kwa Naibu Rais kupata uungwaji mkono kutoka idadi hii ya maseneta.
Upigaji kura katika Bunge la Kitaifa ulishawishiwa na miegemeo ya kivyama na kimaeneo.
Kwa misingi hiyo, inabashiriwa kuwa huenda maseneta 51 wakaunga mkono hoja hiyo huku 12 wakiipinga. Kwa upande mwingine, msimamo wa maseneta wengine wanne haujabainika.
“Ni wazi kuwa maseneta wa chama cha UDA na ambao ni waaminifu kwa Rais William Ruto wataunga mkono hoja hiyo. Aidha, maseneta wa ODM ambao bila shaka ni waaminifu kwa Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga pia wataunga mkono hoja hiyo. Hili lilishuhudiwa katika Bunge la Kitaifa na bila shaka linarejelewa katika Seneti siku ya Alhamisi,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na uongozi Barasa Nyukuri.
“Kwa hivyo, nafasi ya Bw Gachagua kuponea shoka la Seneti ni finyu mnamo. Sababu ni kwamba kwa kiwango kikubwa huu ni mchakato unaoshawishiwa pakubwa na siasa wala sio sheria au uzito wa mashtaka. Tulishuhudia hili wakati wa kuondolewa afisini kwa gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko na Ferdinand Waititu wa Kiambu,” anaongeza.
Ilivyo sasa, chama cha UDA kinachoongozwa na Rais Ruto kinawakilishwa na jumla ya maseneta 34 katika Seneti huku ODM ikiwa na maseneta 20.
Vyama vya Wiper na Jubilee vinawakilishwa na maseneta wanne kila moja, United Democratic Movement (UDM) ina maseneta wawili huku vyama vya Democratic Party, Ford Kenya na National Reconstruction Alliance (NRA) vikiwakilishwa na seneta mmoja kila moja.
Kiongozi wa Wiper ameamuru maseneta wanne wa chama hicho kuangusha hoja hiyo ili kumnusuru Bw Gachagua. Wao ni Enoch Wambua (Kitui), Daniel Maanzo (Makueni), Agnes Kavindu (Machakos) na Seneta Maalum Shakila Abdallah.
Maseneta wa UDA ambao ni wandani wa Bw Gachagua na hivyo wanatarajiwa kuangusha hoja huyo ni James Murango (Kirinyaga), Karungo Wa Thang’wah (Kiambu), Joe Nyutu (Murang’a) na John Methu wa Nyandarua.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba Seneta wa Busia Okiya Omtatah wa chama cha NRA atapinga hoja hiyo ikizingatiwa kuwa amepinga mchakato huo tangu ulipoanza.
Maseneta ambao misimamo yao haujulikani ni pamoja na Tabitha Karanja (Nakuru), John Kinyua (Laikipia), Wahome Wamatinga (Nyeri) na Samson Cherargei wa Nandi .