Huenda Ruto akasuka muungano wa Bonde la Ufa, Nyanza, Magharibi na Pwani Gachagua akipigwa teke
KUUNGANA kwa wabunge walio washirika wa Rais William Ruto na wale wa chama cha ODM kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua kumeibua mipango ya kusuka muungano unaoleta pamoja vigogo wa kisiasa kutoka eneo la Bonde la Ufa, Nyanza na Magharibi.
Tayari, ukuruba wa Rais Ruto na kiongozi wa ODM Raila Odinga umetia doa chama cha United Democratic Alliance baada ya kufaulu kumng’atua Bw Gachagua katika Bunge la Taifa.
Na japo baadhi ya wadadisi wa siasa wanahisi kuwa huenda ukuruba wa Ruto na Raila ulinuiwa kufanikisha kutimuliwa kwa Gachagua, kuna hisia kuwa muungano mkubwa wa kisiasa unasukwa ambao utahusisha vigogo wa kisiasa kutoka Bonde la Ufa, Nyanza na Magharibi pamoja na Pwani.
Muungano huo utakaoleta pamoja, Rais Ruto, Bw Odinga, Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Spika wa Bunge Moses Wetang’ula kwa sasa umechapikwa jina la Western Alliance.
Haikubainika mara moja iwapo wanaosuka muungano huo wana baraka za vigogo hao lakini kulingana na hoja ya kumtimua Gachagua ilivyoshughulikiwa, dalili zinaonyesha kwamba utaiva kabla ya 2027 iwapo hali ya kisiasa haitabadilika.
“Tutakuwa na muungano mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027. Utaleta pamoja vigogo wa kisiasa walio na nia na mawazo sawa ya kupeleka Kenya mbele. Kwa sasa tuko katika awamu za mwanzo ya kuusuka na siwezi kueleza zaidi,” akasema mbunge mmoja kutoka eneo la Magharibi ya Kenya ambaye aliomba tusitaje jina lake kwa kuwa yeye si msemaji wa waandalizi wa muungano huo.
Anasema kuleta upinzani serikalini, na kuunga azma ya Odinga kuwania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika ni sehemu ya maandalizi ya muungano wa Magharibi ambao nguvu zake zilijaribiwa na hoja ya kumtimua Bw Gachagua.
Wengi wa wanachama wa ODM walioteuliwa mawaziri wanatoka eneo la Magharibi, Nyanza na Rift Valley isipokuwa Hassan Joho (Madini) anayetoka Pwani.
Wao ni John Mbadi (Fedha), Opiyo Wandayi ( Kawi), Beatrice Askul (Afrika Mashariki) na Wycliffe Oparanya (Ushirika) Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor.
Wakati wa hoja ya kumtimua Bw Gachagua, wabunge wa ODM, wakiongozwa na kiongozi wa wachache Junet Mohamed waliungana na wale wa Kenya Kwanza.
Vyama vikuu katika Kenya Kwanza ni UDA cha Rais Ruto, Amani National Congress (ANC) cha Musalia Mudavadi na Ford Kenya cha Bw Wetang’ula.
“Rais Ruto anatoka Rift Valley, Raila anatoka Nyanza na Musalia na Wetang’ula wanatoka Magharibi. Huu ni muungano wa Magharibi mwa Kenya ambao mambo yakibaki yalivyo, unaweza kudumu hadi 2027,” asema mdadisi wa siasa Peter Wafula.Hata hivyo, anahisi kuwa huenda ukagawanya nchi hasa kufuatia masaibu yanayomkabili Bw Gachagua anayetoka eneo la Mlima Kenya ambalo limeonyesha dalili za kugawanyika.
“Japo wabunge wengi kutoka Mlima Kenya waliunga hoja ya kumtimua Gachagua, ukweli ni kwamba walitumiwa tu. Baadhi yao hawaelewi mikakati inayoendelea ya kusuka muungano wa Magharibi.
Kwa sasa Mlima Kenya hautakuwa na kigogo wa kisiasa kama maeneo mengine,” asema Wafula.Mdadisi wa siasa Beatrice Kakai anahisi kuwa kuunda muungano wa Magharibi ni sumu kwa utangamano wa nchi.
“Ni sumu kali kwa utangamano wa kisiasa. Itakuwa sawa na kutenga sehemu nyingine za nchi,” asema.
Hata hivyo, Bw Wafula anasema hii ndiyo taswira ya hali ya kisiasa nchini kwa wakati huu.
“Vigogo wa kisiasa kutoka magharibi mwa nchi wameungana. Walipima uwezo wao bungeni wakati wa kumtimua Gachagua ofisini. Iwapo muungano huo utadumu hadi 2027, ni jambo la kusubiri,” akasema.
Aliongeza kuwa wanaosuka muungano huo wanaweza kujumuisha Bw Joho kuwakilisha Pwani, Aden Duale kuwakilisha Kaskazini Mashariki na Alfred Mutua kuwakilisha Kusini Mashariki ili muungano huo “uonekane kuwa na sura ya kitaifa.”