Jamvi La Siasa

Ruto kwa mara nyingine akwepa kuzungumzia masaibu ya Gachagua

Na CECIL ODONGO October 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto Jumapili alikosa kuzungumzia masaibu yanayomwandama Naibu Rais Rigathi Gachagua huku akisema lengo lake la kuhakikisha kuwa taifa lina umoja na usawa kwa wote halitapigwa breki.

Kiongozi wa taifa alizungumzia Bima mpya ya Afya (SHA) ambayo alisema itasaidia kufanikisha mageuzi katika sekta ya Afya na Mradi wa Nyumba za gharama ya chini.

Alisema SHIF itahakikisha kila Mkenya atakuwa na bima ya afya itakayomwezesha kutolipa chochote akifika hospitalini. Tangu SHIF ianze kutekelezwa mnamo Oktoba 1, Wakenya wamekuwa wakilalamikia huduma duni kutokana na kutofanya kazi kwake, baadhi ya hospitali zimelazimika kurejelea bima ya zamani ya NHIF.

“Lengo langu ni kuhakikisha tuna nchi ambapo watu wote wako sawa. Sitaangalia nyuma katika nia yangu ya kuhakikisha hili linatimia,” akasema Rais akiwa katika kanisa la AIC Milimani, Nairobi ambapo aliabudu, akisihi viongozi wa kanisa kumwombea katika kufanikisha hilo.

Hii ni mara ya pili ambapo Rais alikosa kuzungumzia kutimuliwa kwa Bw Gachagua ambaye naye yupo katika Kaunti ya Embu leo Jumapili. Rais alisifu kanisa akisema limechangia mageuzi kwenye sekta ya afya kwa kujenga vituo vya afya maeneo mbalimbali nchini.

Hii ilikuwa mara ya pili Rais alikuwa akihudhuria ibada katika kanisa hilo ambapo alikiri kuwa halikuwa kwenye ratiba yake.

Rais alikuwa akitarajiwa hapo awali kuwahi ibada katika Kaunti ya Embu lakini akafuta ziara hiyo ikikisiwa hatua hiyo ilitokana na suala la kutimuliwa kwa Bw Gachagua kwenye Bunge la Kitaifa.

Aidha, Rais aliahidi kuendeleza juhudi za kusafisha Mto Nairobi, shughuli ambayo alisema itafanikishwa ndani ya miaka miwili.

Pia alitoa wito kwa wanasiasa kutoka Kaunti ya Nairobi waandae mkutano naye ili wapate suluhu kwa suala la zaidi ya wanafunzi 10,000 kutoka kaunti hiyo kuacha shule kutokana na ukosefu wa madarasa.