Kalonzo: Nchi yetu inapigwa mnada kwa usaidizi wa Raila Odinga
KIONGOZI wa chama cha Wiper, Kalonzo Musyoka, amemburura kinara wa Azimio Raila Odinga kwenye mikataba ya mabilioni baina ya serikali na shirika la India, Adani Energy Solutions.
Alisema mikataba hiyo inayohusu sekta za nishati, huduma ya afya na usafiri, ni kiumbe cha serikali pana inayojumuisha serikali ya Kenya Kwanza na wandani wa Bw Odinga.
“Kenya inakabiliwa na tishio la kushikwa mateka huku sekta za kawi, usafiri na afya zikishuhudia serikali ikikabidhi mikataba ya mabilioni kwa Adani kupitia njia isiyo na uwazi. Tutaendelea kupinga mikataba hiyo kortini,” alieleza wanahabari jana Jumapili Nairobi.
Matamshi ya Bw Musyoka yamejiri huku Waziri wa Kawi, Opiyo Wandayi, akifichua kuwa serikali ilitia saini mkataba wa Sh95 bilioni na Adani Energy Solutions kuimarisha usambazaji wa umeme.
Kampuni hiyo ya India inashiriki mazungumzo na serikali kuhusu kuboresha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.
Inasemekana kuwa kampuni hiyo ya India imetia saini mkataba na serikali kuendesha ajenda ya mpango wa afya kwa wote.
“Tunashikilia msimamo wetu kuwa sarakasi zinazozingira kumfurusha Naibu Rais Rigathi Gachagua ni hila zilizodhamiriwa kuwapumbaza Wakenya na kufunika mikataba ya mabilioni inayohusu Adani itiwe sahihi na serikali pana. Tunataka kuwahakikishia Wakenya kuwa hatutaruhusu taifa letu lipigwe mnada na utawala huu,” alisema Bw Musyoka.
Japo alitaja bunge, korti na barabarani kama tasnia zilizopo za kupinga maovu ya serikali, Bw Musyoka aliashiria wazi kwamba hana imani na wabunge na maseneta.
Makamu wa rais huyo wa zamani aliandamana na kiongozi wa chama Democratic Action Party-Kenya, Eugene Wamalwa, Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, na wanasiasa kadhaa wa Wiper.
Aliyekuwa gavana wa Kiambu, Ferdinand Waititu, ni miongoni mwa wanasiasa mashuhuri waliokuwapo lakini ni Bw Musyoka pekee aliyezungumza.
Alikosoa mchakato wa kumfurusha Bw Gachagua ambapo wabunge 282 kutoka kambi zote za kisiasa waliunga mkono mswada huo uliowasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mwengi Mutuse.
“Serikali kwa hakika imeshika mateka bunge. Kama hilo halikuwa wazi hapo mbeleni, matukio ya utimuaji yalithibitisha,” alisema.
Alifichua kuwa chama chake kinatafakari kuwaadhibu wanachama wake waliopiga kura kumng’oa mamlakani Bw Gachagua.