Kalonzo atwaa mwenge wa kiongozi wa upinzani, Raila akiibuka mtetezi sugu wa serikali
KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka sasa anaonekana kutwaa mwenge wa kiongozi wa upinzani kutoka kwa kiongozi wa ODM Raila Odinga kwa kupinga sera za serikali.
Tangu Bw Odinga alipoamua kuungana na Rais William Ruto kurejesha utulivu nchini kufuatia misukosuko iliyosababishwa na maandamano ya Gen-Z Juni na Julai mwaka huu, Bw Musyoka ameendelea kuwaongoza vinara wengine wa Azimio kuukosoa utawala wa Rais William Ruto.
Kwa mfano, makamu huyo wa rais wa zamani amesimama kidete, kupinga mchakato wa kutimuliwa afisini kwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, mpango wa serikali wa ukodishaji wa Uwanja wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) kwa kampuni ya Adani na utekelezaji wa Bima mpya ya Afya ya Kijamii (SHIF).
Aidha, Bw Musyoka amepinga visa vya ukandamizaji wa haki za kimsingi za raia kama vile utekaji nyara mateso na mauaji ya wakosoaji wa serikali, baada ya Bw Odinga “kujiunga” na serikali ya Kenya Kwanza.
Kabla ya hoja ya kumtimua afisini Bw Gachagua kujadiliwa na kupigiwa kura katika Bunge la Kitaifa, Bw Musyoka aliwaagiza wabunge wa Wiper kutoiunga mkono.
“Serikali inatumia mchakato huu usio na maana yoyote kwa Wakenya kukwepa kushughulikia mambo muhimu kwa Wakenya kama vile sakata ya uuzaji uwanja wa JKIA kwa kampuni ya Adani, dosari zilizokumba mfumo mpya wa ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu, bima mpya ya SHIF, migomo ya kila mara ya wafanyakazi miongoni mwa mengine. Kwa hivyo, kama Wiper tunaamuru wabunge wetu wasiunge mkono hoja ya kumwondoa afisini Naibu Rais Rigathi Gachagua,” akasema.
Wabunge wa Wiper, isipokuwa Charles Ngusya (Mwingi Magharibi) na Basil Robert Ngui (Yatta), ni miongoni mwa wabunge 44 waliopinga hoja hiyo iliyodhaminiwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse. Bw Musyoka ameapa kuwaadhibu wawili hawa kwa kukaidi agizo la chama hicho.
Hata baada ya hoja hiyo kupitishwa katika Bunge la Kitaifa na wabunge 282 na kuwasilishwa katika Seneti, Bw Musyoka tena amewaagiza maseneta wanne wa Wiper kuipinga.
Wao ni; Seneta wa Kitui Enoch Wambua, Daniel Maanzo (Makueni), Agnes Kavindu Muthama (Machakos) na Seneta Maalum Shakila Abdallah.
Hatima ya hoja hiyo, inayoungwa mkono na wabunge na maseneta wanaoegemea mrengo wa Rais Ruto na Bw Odinga, itaamuliwa katika Seneti mnamo Alhamisi wiki hii.
Muda mfupi kabla ya Bw Odinga kutetea mpango wa serikali kukodisha uwanjwa wa JKIA kwa kampuni ya Adani na uwekezaji wake katika sekta za kawi na afya, Bw Musyoka alikuwa amemhusisha kiongozi huyo wa ODM na mpango huo.
Alidai Bw Odinga amefaidi kifedha kutokana na mpango huo akiapa kuwasilisha kesi kortini kuupinga.
“Tutaelekea kortini kupinga mpango huu wa utekaji wa mali ya Wakenya, katika sekta za kawi, uchukuzi na afya na kuuziwa Adani kwa mabilioni ya fedha pasina utaratibu wa kisheria kufuatwa,” Bw Musyoka akasema Jumapili kwenye kikao na wanahabari Nairobi.
Aliandamana na vinara wengine wa Azimio kama vile kiongozi wa chama cha Democratic Action Party (DAP-K) Eugene Wamalwa, Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni, Kiongozi wa chama cha Safina miongoni mwa wengine.
Mnamo Septemba 30, mwaka huu, Bw Musyoka alizua kioja katika makao makuu ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) alipotaka yeye na viongozi wenzake wa Azimio waruhusiwe kumwona Gavana wa zamani wa Kiambu Ferdinand Waititu aliyenaswa kwa kutoa matamshi yaliyodaiwa kuwa ya chuki.
Hata hivyo, maafisa wa DCI waliwazuia kumfikia mwanasiasa huyo ambaye ni mwandani wa zamani wa Rais Ruto.
Profesa Gitile Naituli ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, anamshauri Bw Musyoka kuendelea kuwa mtetezi wa umma wakati huu ambapo Bw Odinga anashirikiana na serikali inayounga mkono kampeni zake za kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
“Sasa kile ambacho Kalonzo anasalia kufanya ni kuitisha maandamano makubwa jijini Nairobi na miji mingine nchini kupinga sera mbovu za serikali, ili atwae kabisa nafasi ya Raila,” anaongeza.