Habari za Kitaifa

Kampuni nyingi zilifuta wafanyakazi mwaka huu…lakini benki zikanawiri kunawiri – Utafiti

Na PETER MBURU October 15th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MATOKEO ya utafiti ulioendeshwa katika soko la ajira nchini yanaonyesha kuwa moja kati ya kampuni nne nchini zimewafuta kazi wafanyakazi mwaka huu.

Na ni kampuni moja tu kati ya 10 iliyoajiri wafanyakazi wapya kwa mkataba wa kudumu kuanzia Januari 2024.

Vile vile, licha ya kwamba ni asilimia 13 ya kampuni zimeajiri wafanyakazi wapya vibarua mwaka huu, asilimia 42 ya kampuni za humu nchini zimewafuta kazi wafanyakazi vibarua kutokana na hali ngumu ya kiuchumi.

Utafiti huo uliendeshwa na Benki Kuu Nchini (CBK) mnamo Septemba mwaka huu.

Katika utafiti huo wa kwanza kuendeshwa na benki hiyo kuhusu uajiri na kufutwa kazi kwa wafanyakazi wa viwango tofauti na kampuni, imebainika kuwa kampuni ziliwafuta wafanyakazi wengi mwaka huu kuliko wale ambao ziliweza kuwaajiri.

Utafiti huo unaonyesha kuwa, japo kampuni nyingi zilifuta wafanyakazi ili ziweze kumudu hali ngumu ya kiuchumi tangu Januari mwaka huu, sekta ya benki iliandikisha ustawi. Benki kadhaa ziliendelea kufungua matawi mengi mapya kote nchini.

“Wakuu wa idara husika katika kampuni waliulizwa kuhusu idadi ya wafanyakazi wa kudumu, wale wa kandarasi na vibarua mwaka huu ikilinganishwa na wakati kama huo 2023.

“Majibu yalionyesha kuwa asilimia 59 ya benki zimeajiri wafanyakazi wapya kwa mikataba ya kudumu mwaka wa 2024 huku asasi ambazo mbali na benki zikiajiri asilimia 10 pekee ya wafanyakazi wapya. Aidha, asilimia 25 ya kampuni ambazo haziko katika sekta ya benki zimewafuta kazi wafanyakazi wa kudumu mwaka huu wa 2024 ikilinganishwa na asilimia 4 za benki,” utafiti huo unaonyesha.

Utafiti huo pia ulibaini kuwa asilimia 39 ya benki za humu nchini zimeajiri wafanyakazi wapya kwa kandarasi mwaka huu.