Jamvi La Siasa

Mlima wazidi kuteleza, hatima ya Gachagua kuamuliwa Seneti

Na MARY WANGARI October 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

SENETI itaanza rasmi leo Jumatano vikao vya kusikiza mashtaka yaliyowasilishwa dhidi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua baada ya Mahakama Kuu kukataa ombi la kusimamisha mchakato wa kumng’oa mamlakani.

Kwa mara nyingine tena, jaribio la Bw Gachagua la kuitaka mahakama kusimamisha mchakato ulioanzishwa na Bunge la Kitaifa liliambulia patupu Jumanne, ila Jaji Chacha Mwita akaagiza suala hilo liamuliwe na jopo la majaji watatu watakaotoa uamuzi Jumatano saa mbili asubuhi.

Hata hivyo, inatarajiwa kwamba vikao vya Seneti vitaendelea kama ilivyopangwa.

Wiki iliyopita, Spika wa Seneti Amason Kingi alitangaza kuwa Seneti itashiriki vikao maalum Oktoba 16-17 kusikiza mashtaka 11 yanayomkabili Bw Gachagua.

Kufuatia uamuzi wa mahakama kuu, hatima ya Naibu Rais sasa ipo mikononi mwa maseneta ambao wana muda wa siku kumi kusikiza na kutoa uamuzi wao baada ya kumpa fursa Bw Gachagua kusikizwa.

Ushahidi wa Bw Gachagua uliopakiwa katika masanduku 12 ulisafirishwa Jumatatu kutoka Bungeni hadi Seneti kwa kutumia magari mawili aina ya pickup, katika tukio lililoibua kumbukumbu za kesi ya Azimio ya kupinga matokeo ya urais 2022.

Bw Gachagua aliyetimuliwa baada ya wabunge 282 kupiga kura kuunga mkono hoja ya kumfurusha, alielekea kortini akitumai mchakato huo ungekatizwa na kumpa afueni.

Hata hivyo, akitoa uamuzi wake, Jaji Chacha Mwita alisema korti haiwezi kusimamisha mchakato wa Seneti kwa sababu Katiba imepatia bunge mamlaka ya kuendesha mchakato wa ufurushaji.

Alisema mahakama ni sharti ijizuie kuingilia mchakato huo hadi utakapokamilika katika Seneti na kutoa nafasi ya kuangazia masuala yaliyojitokeza katika kesi hiyo.

“Baada ya kutathmini kesi na hoja kutoka pande husika, katiba na kesi za awali, ombi la kibali cha kusitisha limekataliwa,” alisema Jaji Mwita katika uamuzi wake.

Bw Mwita alihoji kwamba korti haina mamlaka ya kusitisha shughuli hiyo kwa sababu suala hilo lilitokana na mchakato wa kikatiba.

Aidha, aliagiza faili ya Bw Gachagua iwasilishwe mbele ya jopokazi la majaji watatu walioteuliwa na Jaji Mkuu Martha Koome.

Bw Gachagua anayekabiliwa na wakati mgumu aliwasilisha kesi wiki iliyopita akihoji kwamba hoja ya kumtimua ina dosari na inakinzana na mashtaka yaliyowasilishwa mwanzoni dhidi yake.

“Tukisubiri kusikizwa na uamuzi kuhusu kesi iliyowasilishwa, amri inapaswa kutolewa kuzuia na kupiga marufuku Seneti kuendelea na mchakato wa kusikiza mashtaka kuhusu ufurushaji,” alihoji Bw Gachagua.

Jaji mkuu aliteua jopokazi la majaji watatu Eric Ogolla, Antony Mrima na Frida Mugambi kushughulikia suala la kumfurusha Naibu Rais.

Haya yanajiri huku mchakato wa kumtimua Bw Rigathi ukionekana kuendeshwa kwa kasi kupindukia.

Maseneta John Methu (Nyandarua) Samson Cherargei (Nandi) na Enoch Wambua (Kitui) walielezea wasiwasi wao wakisema siku mbili hazitoshi kusikiza mashtaka yote yanayomkabili Naibu Rais.

Spika Kingi alisema Seneti itahakikisha pande zote husika zinapata haki na muda wa kutosha kusikizwa.