Maseneta nao wafuata ‘tabia’ ya wabunge
SENETI Jumanne ilizamika kuahirisha kikao chake kutokana na ukosefu wa idadi hitajika ya maseneta 15 jinsi inavyoamrishwa kwenye katiba.
Seneti ina maseneta 67 na idadi inayohitajika kuendesha shughuli zake ni maseneta 15 na zaidi. Kwa mujibu wa katiba, Bunge la Kitaifa nalo lazima liwe na wabunge 50 au zaidi ili kuendelea na vikao vyake.
Hii ni kinyume na mnamo Jumatatu ambapo maseneta walifika wote wakati wa kujadili hoja ya kumtimua Gavana wa Kericho Erick Mutai.
Kukosekana kwa idadi inayofaa ya maseneta kulitokea wiki moja baada ya Bunge la Kitaifa nalo kulazimika kutoendelea na vikao vyake kwa kuwa wabunge hawakuwepo.
Kinaya ni kuwa wakati wa kujadili na kuipigia kura hoja ya kumtimua Naibu Rais Rigathi Gachagua, wabunge 326 walikuwepo.
Siku hiyo hata kengele ambayo Naibu Spika Gladys Shollei aliamrisha ipigwe haikusaidia kitu kwa sababu wabunge hawakuwepo.
Jana, seneti ilifuata mkondo, kwa kuwa kulikuwa na chini ya maseneta 10 wakati wa kikao cha asubuhi. Licha ya Naibu Spika Kathuri Murungi kuamrisha kengele ipigwe kuwaamrisha maseneta waje kikaoni, bado idadi hitajika haikufika.
“Waheshimiwa maseneta, kutokana na kutotimia kwa idadi hitajika ya maseneta, naahirisha kikao hadi saa 2.30 leo (jana),” Bw Murungi akasema akiahirisha kikao cha jana.
Seneti ilikuwa imeorodhesha kusomwa kwa hoja 14 na miswada mitatu. Pia kulikuwa na miswada mitatu ambayo ilikuwa iangaziwe kwa sababu ilipendekezewa ifanyiwe marekebisho.
Miswada hiyo ilikuwa ni Mswada wa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa 2023 na Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi, ambayo inadhaminiwa na Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot.
Pia kulikuwa na Mswada wa Kuzuia na Kudhibiti Saratani 2023 ambao unadhaminiwa na Seneta wa Nandi Samson Cherarkey.
Miswada mingine ambayo ilikuwa iangaziwe ni Usimamizi wa Fedha za Umma (Seneta Hamida Kibwana), Huduma za Dharura za Uokoaji wakati wa Moto 2023 (Mohamed Abass) na Uchukuzi wa Umma 2023 (Bonny Khalwale).
Miswada mitatu kuhusu Ripoti ya Maridhiano Nchini (NADCO), Mswada wa Vyama vya Kisiasa na Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Uchaguzi 2024 pia ilikuwa iangaziwe.
Kulikuwa na ripoti kadhaa za uchunguzi kutoka kwa kamati ambazo zilikuwa ziwasilishwe.
Kati ya ripoti hizo ni uajiri katika idara mbalimbali za serikali, kurefushwa kwa mikataba ya ununuzi na kusambazwa kwa kawi nchini, ripoti kuhusu mlipuko wa gesi Embakasi na pia kudadavuliwa kwa ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali kuhusu matumizi ya fedha kwenye kaunti.
Hatua ya wabunge na maseneta kukosa kufika bungeni inaonyesha kuwa hawachukulii kwa uzito kazi zao.
Mwaka jana Bw Cheruiyot aliwachemkia maseneta, akisema anashangaa kwa nini wanapigania wachaguliwe kisha mwishowe wanatelekeza majukumu yao waliyopewa na Wakenya.