Jamvi La Siasa

Gachagua aonekana kuishiwa na mbinu ombi la kuzima Orengo na ushahidi mpya likitupwa na Spika

Na MARY WANGARI October 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NAIBU Rais, Rigathi Gachagua Jumatano alipata pigo la mapema, wakati Spika wa Seneti Amason Kingi alipotupilia mbali ombi la kuondoa Gavana wa Siaya James Orengo kutoka kwa orodha ya mawakili wa upande wa mashtaka.

Aidha, Spika Kingi vile vile alikataa ombi la mawakili wa Bw Gachagua la kuondoa ushahidi mpya waliosema umeletwa baada ya dirisha la kuandikisha ushahidi kufungwa.

Kupitia hoja ya kumfurusha Naibu Rais iliyowasilishwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi, Mutuse Mwengi, Bw Gachagua anakabiliwa na madai yanayojumuisha kuhujumu umoja wa kitaifa na kuchochea ukabila kupitia matamshi yanayosababisha migawanyiko.

Anasemekana pia kutelekeza majukumu yake kama Naibu Rais na kwenda kinyume na sera za serikali hivyo kukiuka kanuni kuhusu uwajibikaji wa pamoja.

Isitoshe, anadaiwa kuhujumu ugatuzi kwa kuingilia shughuli za kaunti, kutishia na kuhujumu kanuni kuhusu uhuru wa mahakama.

“Matamshi ya Gachagua kwa jumla yanaenda kinyume na sera tulizobuni kwa pamoja kama serikali hivyo kuvuruga uadilifu wetu,” alihoji Bw Mutuse Mwengi kupitia hoja ya utimuaji.

Kulingana na naye, matamshi ya Bw Gachagua,” yanachochea migawanyiko na kuhujumu kanuni za kimsingi za Katiba yetu, ikiwemo umoja na ujumuishaji.”

Hata hivyo, Bw Gachagua alipofika mbele ya Seneti katika kikao cha kwanza kuhusu mchakato wa kumtimua, alikanusha mashtaka yote aliyosomewa na karani wa Bunge la Seneti, Jeremiah Nyengenye na kusema hana hatia.

Haya yalijiri huku Bw Gachagua akionekana kuishiwa na mbinu baada ya kuwasilisha, bila kufua dafu,  jumla ya kesi 26 katika jaribio la kuzuia mchakato wa Seneti kumfurusha.

Katika muda wa saa kadhaa kati ya Jumanne na Jumatano, kesi mbili mpya zilizowasilishwa na Naibu Rais kwa matumaini ya kukatiza mchakato huo ziliambulia patupu.

Jumatano asubuhi, jopokazi la majaji watatu lililoteuliwa na Jaji Mkuu Martha Koome lilitupilia mbali ombi la Bw Gachagua la kuzima mchakato wa kumfurusha katika Seneti.

Majaji Freda Mugambi, Eric Ogolla na Anthony Mrima walisema kwa manufaa ya umma, mchakato huo wa kikatiba unapaswa kuendelea bila kutatizwa.

“Hoja kwamba mlalamishi anakoma kuongoza afisi baada ya kufurushwa, tunahoji kuwa kila afisa anaweza tu kurejea afisini kisheria na kikatiba. Karani wa korti anaweza kushughulikia hili katika hatua yoyote,” walisema.

Uamuzi huo ulitolewa hata kabla ya timu inayomwakilisha Naibu Rais kupata afueni kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu ulioruhusu Seneti kuanza rasmi mchakato wa ufurushaji baada ya kukataa ombi la kuusimamisha.

Jaji Chacha Mwita alisema katiba imepatia bunge mamlaka ya kuendesha mchakato wa ufurushaji hivyo korti haiwezi kusimamisha Seneti.

Alisema mahakama ni sharti ijizuie kuingilia mchakato wa Seneti hadi utakapokamilika ili kutoa nafasi ya kuangazia masuala yatakayoibuka akisema suala hilo lilitokana na mchakato wa kikatiba.

Naibu Rais aliwasilisha kesi wiki iliyopita akihoji kwamba hoja ya kumtimua ina dosari na inakinzana na mashtaka ya awali yaliyowasilishwa dhidi yake.

“Tukisubiri kusikizwa na uamuzi kuhusu kesi iliyowasilishwa, amri inapaswa kutolewa kuzuia na kupiga marufuku Seneti kuendelea na mchakato wa kusikiza mashtaka kuhusu ufurushaji,” alihoji Bw Gachagua.