Habari za Kitaifa

Hali si nzuri, achana na Adani, urudishe NHIF, viongozi wa kidini wamsihi Ruto

Na KEVIN CHERUIYOT October 17th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

VIONGOZI wa kidini sasa wanasema nchi inaelekea pabaya huku Wakenya wakizidi kutatizwa na Bima Mpya ya Afya ya Kijamii (SHA) huku Rais William Ruto akisalia kimya kuhusu mchakato unaoendelea wa kumng’óa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Wakizungumza chini ya Baraza la Kitaifa la Makanisa Nchini (NCCK), viongozi hao walimtaka Rais Ruto azinduke na kukabiliana na matatizo yanayozonga nchi, wakisema mengi yanaweza kusuluhishwa.

Walisema kuwa vifo vimeanza kushuhudiwa wakati wa kuhamisha Wakenya kutoka Hazina ya Bima ya Kitaifa ya Afya (NHIF) hadi SHA.

“Kwani ni lazima Wakenya walipe mabilioni kwa mabroka ambao hawaongezi chochote kuhusu huduma za afya nchini? Wakenya sasa wanahitajika kulipa pesa nyingi zaidi kwa SHA ilhali sisi tunapendekeza turejelee NHIF,” ikasema taarifa yao.

Rais Ruto pia alikashifiwa kwa kushinikiza mwongozo mpya wa ufadhili katika vyuo vikuu, ambao umewazuia wengi kujiunga na vyuo hivyo kwa kushindwa kumudu karo.

“Elimu kwa Wakenya imevurugwa kutokana na mabadiliko katika mwongozo wa ufadhili wa elimu ya vyuo vikuu. Tunaomba mwongozo huu mpya wa ufadhili uondolewe kupisha mashauriano zaidi ndipo kuwe na haki na usawa kwa wanafunzi wote,” wakasema viongozi hao wa kidini.

Kwao, Rais hakuwapa ufafanuzi wowote kwa nini mfumo wa awali uliondolewa ilhali haukuwa na tatizo lolote.

Kuhusu kutimuliwa kwa Bw Gachagua, viongozi hao, walisema mchakato umefuata sheria ila wakazua maswali kuhusu kimya cha Rais Ruto, wakisema kinasababisha taharuki.

“Tunatoa wito kwa Rais Ruto azungumzie suala hili la kutimuliwa kwa Naibu Rais. Hili ni suala ambalo linahusisha umma na pia msaidizi wa Rais na Wakenya wana haki ya kujua msimamo wa Rais,” wakasema.

Viongozi hao pia walitoa wito wa kufutiliwa mbali kwa kandarasi zote ambazo zimetolewa kwa kampuni kutoka India ya Adani, wakisema mchakato wa kuridhisha wa utoaji zabuni haukufuatwa.

Walisema shughuli za kampuni hiyo zinazua shauku hasa katika nchi ambayo imelaumiwa kwa kutofanya vizuri kwenye sekta ya uwekezaji kama India, Australia na Bangladesh.

“Futilia mbali kandarasi zote ambazo zimepewa Adani na kampuni zake katika sekta ya afya, kusambaza umeme na usimamizi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta,” akasema.

Bunge pia lilishauriwa liondoe miswada yote ambayo hainufaishi raia kama ile ya kilimo na ile inayopendekeza kuongezwa kwa muhula wa viongozi waliochaguliwa.

“Wabunge wanastahili kuwahudumia Wakenya ama wajiuzulu kwa sababu hawatimizi maslahi ya raia tena,” ikasema taarifa hiyo.

Kando na hayo viongozi hao wa kidini walidai kuna ufisadi kwenye sekta mbalimbali hasa katika serikali kuu na za kaunti huku ahadi ambazo zilitolewa na serikali zikikosa kutimizwa.

Taarifa hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa NCCK Dkt Elias Agol Kasisi Peter Kamomoe na Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Waislamu na Maimamu Muhdhar Ahmed.